Iran : Mazungumzo ya nyuklia yumkini kurefushwa
23 Novemba 2014Kufuatia juhudi za kidiplomasia za miaka kadhaa Iran na mataifa sita yenye nguvu duniani wameipanga tarehe 24 Novemba kuwa siku ya mwisho ya kufikia makubaliano ambayo yatapunguza shughuli za nyuklia za Iran kwa miaka mingi ili nchi hiyo iweze kuondolewa vikwazo ilivyowekewa.
Duru za Iran zimekaririwa zikisema "Kwa sababu ya ukosefu wa muda na masuala mengi yaliokosa ufumbuzi yumkini ikawa vigumu kufikia makubaliano kamili hapo Jumatatu."
Kwa mujibu wa mjumbe wa mazungumzo hayo wa Iran mazungumzo hayo yanayofanyika katika mji mkuu wa Austria Vienna yanaweza yakabadili mwelekeo na kujikita katika kufikia makubaliano ya kawaida na masuala mengine kuja kupatiwa ufafanuzi hapo baadae.
Mawaziri wa mambo ya nje waliokuwa na mazungumzo yaliochukuwa muda mrefu katika mji mkuu wa Austria Vienna wamekwama katika juhudi zao za makubaliano kabambe kufikia hapo Jumatatu.
Tafauti kuu mbili
Pande zote mbili bado zinatafautiana sana katika masuala mawili makuu ,Iran itaruhusiwa kurutubisha madini ya urani kwa kiwango gani na vikwazo dhidi xs nchi hiyo vitaondolewa kwa muda gani.
Baadhi ya wajumbe katika mazungumzo hayo pia wamezungumzia uwezekano wa kurefusha makubaliano yaliopo hivi sasa ambayo yamefikiwa na Iran na mataifa hayo sita mwaka mmoja uliopita mjini Geneva ili kuwa na msingi wa kuendelea na mazungumzo hayo hadi kufikia makubaliano ya mwisho.
Chini ya makubaliano hayo ya kujenga kuaminiana yaliofikiwa Geneva Iran imesitisha kutanua mpango wake huo wa nyuklia na ikaondolewa baadhi ya vikwazo.
Wanadiplomasia zaidi kushiriki
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry,Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif na Catherine Ashton msuluhishi mkuu wa mataifa sita hapo Jumamosi walikuwa na mkutano wa masaa mawili mjini Vienna.
Wanadiplomasia wengine wakuu wa mataifa hayo sita yenye nguvu wanatarajiwa kuwasili mjini humo leo usiku na mapema hapo Jumatatu.Kundi hilo la mataifa sita yenye nguvu duniani linajumuisha Uingereza, China, Ufaransa, Urusi,Marekani na Ujerumani.
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Saud- Faisal amekutana na Kerry Jumapili mjini Vienna kushauriana juu ya suala la hadhi ya mazungumzo hayo.Mataifa ya Ghuba na Israel yana wasi wasi ule ule waliokuwa nao mataifa ya magharibi kwamba mpango wa nyuklia wa Iran utatumika kutengenezea silaha za nyuklia.Viongozi wa Iran wanasema mpango huo ni kwa ajili tu ya kuzalisha nishati na matumizi ya kisayansi.
Afadhali kutokuwa na makubaliano
Kufuatia mazungumzo yake ya simu na Kerry Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema ni afadhali kutokuwa na makubaliano kabisa kuliko kuwa na makubaliano mabaya ambayo yataweka hatarini Israel, Mashariki ya Kati na ubinaadamu wote.
Makubaliano yanatazamiwa kumaliza mzozo wa miaka 12 kati ya Iran na mataifa ya magharibi ambayo yalizusha uwezekano wa Israel kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani amesema lengo linabakia pale pale kufikia makubaliano hayo Jumatatu usiku lakini wanajadili na washirika wenzao wa ndani na nje ya nchi maamuzi mengine mbali mbali.
Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/AFP
Mhariri : Caro Robi