1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kutotekeleza ahadi za nyuklia

8 Mei 2019

Wizara ya mambo ya nje ya Iran imesema Jamhuri hiyo ya Kiislamu imeamua kusimamisha utekelezaji wa baadhi ya ahadi ilizotoa katika mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 iliyotia saini na mataifa yenye nguvu zaidi duniani.

https://p.dw.com/p/3I7To
Irak Staatsbesuch Hassan Rohani
Picha: picture-alliance/AA/Iranian Presidency

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif amesema hatua ambazo Marekani imechukua katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita baada ya kujiondoa kutoka kwenye mkataba huo na hata kabla kujiondoa, ni ishara ya wazi ya kuzuia kuendelea kuwepo kwa mkataba huo.

"Vifungu vya 26 na 36 vya mkataba wa nyuklia vimeipa Iran pamoja na nchi nyengine zilizotia saini uwezo wa kusimamisha utekelezaji wa ahadi zao kwa sehemu fulani au kikamilifu. Hii ni iwapo mojawapo ya nchi zitakataa kutekeleza ahadi zake. Kwa hiyo Iran haijakiuka chochote kwa kuchukua hatua hii," alisema Zarif.

Iran imetuma barua kwa nchi zilizotia saini mkataba wa 2015

Chini ya mkataba huo wa mwaka 2015 Iran iliondolewa baadhi ya vikwazo kwa masharti ya kusitisha uendelezaji wa mpango wake wa nyuklia. Baada ya Marekani kujiondoa kutoka kwenye mkataba huo ilivirejesha vikwazo kwa Iran, jambo lililochochea mzozo wa kiuchumi nchini humo kuwa mbaya zaidi.

Iran, Außenminister Mohammad Javad Zarif
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad ZarifPicha: Isna

Iran imetuma barua kuhusiana na uamuzi wake kwa viongozi wa Uingereza, China, Umoja wa Ulaya, Ufaransa na Ujerumani. Nchi zote hizo zilikuwa miongoni mwa nchi zilizotia saini mkataba huo na bado zinaendelea kuunga mkono. Barua moja pia itatumwa kwa Urusi.

Hakujakuwa na jawabu kutoka kwa Marekani ingawa Jumapili ilisema kwamba itatuma meli yenye uwezo wa kubeba ndege na silaha yenye uwezo wa kurusha makombora umbali mrefu katika ghuba ya Uajemi kutokana na kile ilichokielezea kama kitisho kipya kutoka kwa Iran.

Iran haitauza tena urani kwa nchi za nje

China imesema mkataba huo wa nyuklia ni sharti uungwe mkono kikamilifu. Israel nayo kupitia kwa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu imesema haitokubali kamwe Iran kuendelea na utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Russlands Präsident Putin trifft sich mit dem israelischen Präsidenten Benjamin Netanjahu
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS.com/A. Druzhinin

Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema Jumatano hawataziuzia tena nchi za nje, urani na maji ya kutengeneza silaha za nyuklia, kama ilivyoainishwa kwenye mkataba huo wa mwaka 2015. Rouhani ametoa muda wa mwisho wa siku sitini ili kupatikana kwa maelewano mapya katika mkataba huo.

Matamshi haya ya Rouhani yamekuja wakati umetimia mwaka mmoja kamili tangu Rais Donald Trump wa Marekani alipotangaza uamuzi wa kuiondoa Marekani kutoka kwenye mkataba huo.