1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kutathmini Uhusiano wake na IAEA

3 Desemba 2009

Hatua hiyo kuzilenga nchi zilizopiga kura kuunga mkono Azimio dhidi yake.

https://p.dw.com/p/KpmM

Spika wa Bunge la Iran amesema kwamba bunge la Jamhuri hiyo ya Kiislamu litautathimini upya uhusiano na nchi zilizopiga kura dhidi ya mpango wake wa Kinyuklia wakati wa kikao cha Shirika la nguvu za Atomiki la Umoja wa mataifa-IAEA- wiki iliopita ilikuwa na ushirikiano mzuri na bodi ya magavana ya Shirika hilo , lakini azimio la hivi karibuni linazusha haja ya kutathminiwa kwa makini kura iliopigwa katika bodi hiyo.Akaongeza kwamba kamati ya bunge ya usalama wa taifa itachunguza uhusiano wa Iran na nchi zilizopiga kura kuliunga mkono azimio dhidi yake.

Shirika hilo lilikasirishwa wiki iliopita na hatua ya Iran ya kuficha juu ya ujenzi wa kiwanda cha pili cha kurutubisha madini ya uranium karibu na mji mtakatifu wa Qom, kuongeza idadi ya kile cha kwanza kilichoko Nantaz, huku Shirika hilo likiitaka Iran isitishe mpango wake huo wa nyuklia.

Nuklearanlage im Iran
Eneo moja wapo katika mradi wa Kinyuklia wa Iran hukoPicha: AP

Azimio hilo lilipitishwa na nchi 25 , tatu zilipinga na 6 hazikupiga kura na likaungwa mkono hata na Urusi na China katika tukio ambalo ni nadra panapohusika na msimamo wao kuelekea Iran.

Larjani alisema Iran inasimama kidete katika lengo lake na kuwa madai ya nchi za magharibi kwamba ina lengo la kuunda silaha za Kinuklia ni uwongo mtupu, akisisitiza kuwa mpango huo ni kwa ajili ya matumizi ya nishati pekee.

Jumapili iliopita, mvutano huo ukaingia katika sura nyengine, baada ya Iran kutangaza kwamba itajenga viwanda vyengine 10 vya kurutubisha madini ya uranium, ikiwa ni kulipiza kisasi kwa kura iliopigwa na Shirika la nguvu za atomiki la Umoja wa mataifa.

Wakati huo huo Mwanasiasa mwenye usemi nchini humo ambaye ni rais wa zamani Akbar Hashemi Rafsanjani ameyataka makundi yote ya kisiasa nchini Iran kuwa pamoja kukabiliana na shinikizo la nchi za nje kuhusu mpango wa kinuklea wa nchi hiyo. Akaonya kwamba inaelekea kuna maridhiano yaliofikiwa kuiabana Iran na kuinyima haki ya kinyuklia.

Nayo Syria jana ilirudia tena msimamo wake wa kuiunga mkono Iran ikisema ina haki ya kuwa na teknolojia ya Kinyuklia. Akizungumza mjini Damascus jana baada ya kukutana na Katibu wa baraza la usalama wa taifa la Iran Saed Jalili, Rais wa Syria Hafidh al-Assad alisema ni haki ya Iran kuwa na teknolojia ya Kinyuklia kwa madhumuni ya amani.

Marekani na nchi shirika zimetishia kushinikiza vikwazo zaidi vya Umoja wa mataiafa dhidi ya Iran ikiwa itakataa kuheshimu matakwa ya jumuiya ya kimataiafa kuhusiana na mpango wake huo wa Kinyuklia. Mapema wiki hii, rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran alisema vikwazo havitatoa mtokeo yoyote.

Mwandishi: M.Abdul-Rahman

Mhariri:Oummilkheir Hamidou