1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran kuongeza uwezo wake wa kuboresha madini ya Urani

6 Juni 2018

Ufaransa yasema tamko la Iran juu ya uboreshaji wa madini ya Urani ikiwa makubaliano ya mpango wake wa nyuklia yatasambaratika ni hatua ambayo itafikia kuuvuka "mstari mwekundu".

https://p.dw.com/p/2z0rQ
Iran Treffen zwischen Chamenei und Studenten
Picha: Irna

Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian amesema daima ni hatari kujaribu kuvuka mipaka iliyowekwa. Le Drian hata hivyo amesema mikakati ya kuyaokoa makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran bado iko imara.

Iran imetoa taarifa kwa Umoja wa Mataifa juu ya mipango yake ya kuongeza kiwango cha kurutubisha madini ya Urani kulingana na makubaliano yaliyoafikiwa mnamo mwaka 2015 baina yake na mataifa makubwa ya dunia. Iran inachukua hatua hiyo wakati ambapo pana hali ya wasiwasi juu ya mustakabali wa mkataba ya kihistoria ulioafikiwa baina yake na mataifa hayo makubwa juu ya mpango wake wa nyuklia.

Msemaji wa shirika la nishati ya nyuklia la Iran Behrouz Kamalvandi amenukuliwa na vyombo vya habari vya nchini mwake akisema kuwa Iran imewasilisha barua kwa shirika la kimataifa la nishati ya nyuklia IAEA inayofafanua juu ya hatua yake. Hali hiyo ya wasiwasi kati ya Iran na nchi za Magharibi imezuka upya baada ya Rais wa Marekani Donald Trump mwezi uliopita kutangaza kuwa ameiondoa nchi yake kwenye makubaliano hayo yaliyofikiwa mnamo mwaka 2015.

Wakati huo huo mkurugenzi wa mpango wa nyuklia wa Iran, Ali Akbar Salehi amethibitisha kuwa nchi yake imeshaanza kazi ya kuikarabati mitambo ya kurutubisha madini ya Urani kwenye kituo chake cha Natanz.

Mkurugenzi wa mpango wa nyuklia wa Iran Ali Akbar Salehi
Mkurugenzi wa mpango wa nyuklia wa Iran Ali Akbar SalehiPicha: tasnim

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu anakabiliwa na upinzani katika miji mikuu ya Ulaya wakati huu anapofanya ziara barani Ulaya na wanaompinga wanasema ni kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya Iran. Netanyahu leo amekutana na waziri wa Fedha wa Ufaransa Bruno Le Maire, ambaye anasisitiza kudumisha uhusiano wa kibiashara kati ya Ulaya na Iran ulioruhusiwa chini ya makubaliano ya mwaka 2015 yanayolenga kuizuia Iran kuendelea na shughuli za mpango wake wa nyuklia.

Mapema wiki hii, Netanyahu alikutana na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, ambao wote wawili walisisitiza kuwa wanaunga mkono mkataba huo uliofikiwa kati ya Iran na nchi zenye nguvu makubaliano ambayo Netanyahu anasema ni mepesi mno kupewa nchi kama Iran.

Baadaye leo Netanyahu ataelekea mjini London kukutana na waziri mkuu wa Uingereza Theresa May na waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson. Netanyahu amesema lengo lake kuu kwa sasa ni jinsi ya kuyashinikiza majeshi ya Iran yaondoke kutoka nchini Syria.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/APE

Mhariri:Josephat Charo