Iran ina nguvu zaidi kuliko wakati wa vita na Iraq-Rouhani
11 Februari 2019Wairan wako kwenye maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 40 ya mapinduzi ya kiislamu yaliyouangusha utawala wa Shah Mohammed Reza Pahlavi uliokuwa ukiungwa mkono na Marekani.Ujumbe mkubwa uliotolewa na kiongozi wa jamhuri hiyo ya kiislamu umesisitiza kwamba nchi hiyo haitompigia mtu yoyote magoti au kuomba ridhaa ya mtu kuendelea na harakati zake za kujiimarisha kijeshi.
Hotuba ya rais Rouhani imetilia mkazo kwamba njama zinazofanywa na adui dhidi ya Iran zitashindwa kwa namna zote.Na kuonya kwamba sasa nchi hiyo ya Jamhuri ya kiislamu ina nguvu kubwa zaidi kuliko wakati ilipopambana na Saddam Hussein wa Iraq katika vita vilivyosababisha maafa makubwa na uharibifu kutoka mwaka 1980 mpaka 1988.
Rouhani amesema leo hii ulimwengu unapaswa kutambua kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uwezo mkubwa zaidi kuliko siku za vita. Pia ameipuuza miito kutoka Marekani na Ulaya ya kutaka pafanyike makubalino mapya ya kuuzuia mpango wake wa Nuklia.
''Mwaka huu tunasherehekea miaka 40 ya kinachoangaliwa kama siku ya ushindi katika mapinduzi ya kiislamu ya mwaka 1979 ya nchi yetu dhidi ya njama za wahalifu Wamarekani,wazayuni na nchi zilizopitwa na wakati za kanda hii ambazo zinataka kuwaangusha watu wetu kupitia shinikizo na vikwazo. Leo uwepo wa umma mitaani katika sherehe hizi za kumbukumbu kote nchini kunamaanisha kwamba njama za maadui zimeshindwa. Uwepo huu unamaanisha kwamba adui hatofanikiwa katika malengo yake ya uovu''
Rouhani pia ameipuuza miito kutoka Marekani na Ulaya ya kutaka pafanyike makubalino mapya ya kuuzuia mpango wake wa Nuklia.Lakini kwa upande mwingine Kamanda wa ngazi ya juu katika jeshi la kimapinduzi la Iran amenukuliwa akisema nchi hiyo itaiangamiza kabisa miji ya Israel ya Haifa na Tel Aviv ikiwa Marekani itaishambilia jamhuri hiyo ya kiislamu. Sambamba na hayo miji mbali mbali ya Iran ilifurika umati wa watu kuanzia Abadan kusiniMagharibi mwa Iran mpaka Mashad kaskazini mashariki mwa nchi hiyo wakisikika wakipaaza sauti za kuilaani Marekani. Kiongozi wa juu wa sasa Ayatollah Ali Khamenei anatajwa kujiandaa kutowa taarifa ya kina yenye malezo kuhusu hatua ya pili ya kuendeleza mapinduzi ya kiislamu.
Mwandishi:Saumu Yusuf /AFP/APE
Mhariri:Josephat Charo