Iran: Ayatollah Khamenei aunga mkono harakati za Wahouthi
14 Agosti 2019Kiongozi huyo mkuu wa kidini Ayatollah Ali Khamenei alimkaribisha msemaji wa waasi wa Houthi, Mohammed Abdul Salam nyumbani kwake mjini Tehran siku ya Jumanne. Kiongozi huyo Khamenei amesema Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu na wafuasi wao wamefanya uhalifu mkubwa nchini Yemen. Amesema nia yao kuu ni kuigawa Yemen. Khamenei ameongeza kusema kwamba njama hii inapaswa kupingwa na Yemen huru yenye umoja na uadilifu.
Kiongozi huyo mkuu pia amefanya mazungumzo na kiongozi wa juu wa waasi wa Yemen siku chache baada ya Saudi Arabia na washirika wake wa Umoja wa Falme za Kiarabu kuingia kwenye malumbano baada ya waasi wanaotaka kujitenga wa kusini mwa Yemen wanoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu kuuteka mji mkuu wa pili wa Yemen, Aden siku ya Jumamosi.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umekuwa ukipambana na waasi wa Houthi kwa muda wa miaka minne sasa katika jitihada za kuirudishia serikali ya Yemen mamlaka kamili. Maelfu ya watu wameuawa na wengi wao wanakabiliwa na umasikini mkubwa pamoja na hali mbaya ya ukosefu wa chakula.Wahouthi ambao wanaudhibiti mji mkuu, Sanaa na maeneo mengi yaliyo na idadi kubwa ya wakaazi wameongeza mashambulio katika miezi ya hivi karibuni dhidi ya Saudi Arabia, nchi ambayo ni hasimu mkubwa wa Iran. Mashambulio hayo ni hatua ya kujibu mashambulizi yanayofanywa na vikosi vya muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya maeneo ya maeneo ya kijeshi ya wahouthi hasa katika maeneo yaliyo karibu na mji mkuu Sanaa.
Ijapokuwa Riyadh na Abu Dhabi zinataka kuonyesha kuwa zina umoja juu ya Yemen, lakini kutekwa mji wa Aden na waasi wanaoungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu kunafichua mgawanyiko kati ya pande hizo mbili jambo ambalo wachambuzi wanasema linadhoofisha kampeni yao ya pamoja dhidi ya waasi wanaoungwa mkono na Iran.
Kutekwa kwa kasri la Rais katika mji wa kusini wa bandari siku ya Jumamosi ni pigo jipya kwa Saudi Arabia, ambayo operesheni yake ya kijeshi haijafaulu kuwashinda waasi wa Houthi na badala yake imesababisha mzozo wa kibinadamu nchini Yemen.
Vyanzo: RTRE/AFP