1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Irak:Tume ya uchaguzi yawekwa chini ya Mahakama

7 Juni 2018

Tume huru ya uchaguzi ya nchini Irak imesema itakata rufaa baada ya bunge kupitsha sheria ya kuhesabiwa upya kura za uchaguzi uliofanyika tarehe 12 mwezi Mei na kusimamishwa kwa tume hiyo ya uchaguzi.

https://p.dw.com/p/2z6A2
Irak, Bagdad: Radikale Shiiten ehren Majid Kassim
Picha: picture-alliance/K. Kadim

Sadr, mwanasiasa anayefuata nadhari za kizalendo alitumia chuki inayozidi dhidi ya Iran, kujinyakulia ushindi wa kushangaza katika uchaguzi wa Mei 12 kwa kuahidi kupambana dhidi ya rushwa na kuboresha huduma za kijamii. Amesema katika taarifa kuwa kamati itaundwa kuchunguza mripuko huo, na matokeo ya uchunguzi huo kuwekwa wazi katika muda wa siku tatu. Ametoa wito wa utulivu na kujizuwia.

Watu wasiopungua 18 wameuawa na zaidi ya 90 kujeruhiwa katika mji wa Sadr, katika mripuko huo ambao wizara ya mambo ya ndani imesema umetokana na kuripuka kwa shehena ya silaha. Waziri Mkuu Heidar al- Abadi amesema katika taarifa kuwa kuhifadhi silaha katika maeneo ya wakaazi ni kosa la uhalifu na ameiagiza wizara ya ndani kuchunguza tukio hilo na kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya wahusika.

Imamu wa Kishia wa Irak Muqtada al-Sadr
Imamu wa Kishia wa Irak Muqtada al-SadrPicha: picture-alliance/K. Kadim

Baadhi ya wapinzani wa kisiasa wa al-Sadr wamesema kupitia mitandao ya kijamii kuwa shehena hiyo ya silaha ilikuwa inamilikiwa na kundi lake la wapiganaji la Saraya al-Salam. Saa kadhaa kabla ya mrupiko huo, bunge la Iraq lilipitisha sheria na kuamuru kuhesabiwa upya kwa mkono, kura za uchaguzi wa bunge, siku moja baada ya Abadi kusema kulikuwepo na ukiukaji mkubwa.

Bunge hilo liliivunja tume ya uchaguzi na kuwapa majaji jukumu la kuhesabu upya kura zote milioni 11 zilizopigwa katika uchaguzi huo. Msaidizi wa juu wa Sadr Dhiaa al Asadi alisema katika ujumbe wa twitter kwamba wakati udanganyifu wowote au ukiukaji katika mchakato wa uchaguzi unapaswa kulaaniwa, suala hilo linapaswa kushughulikiwa na tume huru ya uchaguzi na mahakama ya shirikisho. Ameelezea wasiwasi pia kwamba baadhi ya vyama vya siasa vilikuwa vinajaribu kuhujumu ushindi wa Sadr.

Msemaji wa baraza la mahakama kuu Abdul-Sattar Bayrkdar amesema wanasheria wa juu waliochaguliwa na bunge, watakutana siku ya Jumapili ili kuchagua majaji ambao wataendesha tume na kusimamia zoezi jipya la kuhesabu kura kama ilivyoamriwa na sheria za nchi hiyo. Bayrkdar amesema kuwa tume hiyo mpya  itatenda kazi zake kwa njia nzuri na itakayozingatia haki.

Migawanyiko kati ya raia wa Irak wa madhehebu ya Sunni na wenzao wa madhehebu ya Shia ambao ni wengi iliongezeka baada ya uvamizi ulioongozwa wa Marekani wa mwaka 2003 na ndiyo sababu hasa ya vurugu ziliyofuatiwa na uvamizi na hatimaye kupata nguvu kwa kundi lenye itikadi kali za Kiislam la IS.

Waziri mkuu wa Irak  Haider al-Abadi
Waziri mkuu wa Irak Haider al-AbadiPicha: picture-alliance/dpa/AP

Kwa sasa matatizo hayo yanaonekana yamepungua hasa baada ya vita dhidi ya IS na hata  wanasiasa wengi wa Kishia walionekana wakifanya kampeni waziwazi katika maeneo ya Wasunni.

Ni idadi ndogo tu ya wapiga kura ndio walioshiriki kwenye uchaguzi huo wa mwezi uliopita wa nne kufanyika katika kipindi cha miaka 15 iliyopita. Pia uligubikwa na hasira kutokana na wanasiasa kushindwa kuleta maendeleo na kuonekana kana kwamba hawapo kabisa.

Wafuasi wa kiongozi wa Kishia mwenye msimamo mkali Muqtada al-Sadr, ambaye wakati mmoja aliongoza mapambano dhidi ya majeshi ya Marekani, walipata ushindi wa viti vingi, wakifuatiwa na ushirikiano wa vikosi vya kijeshi vya Kishia na kikosi kingine kinachoongozwa na waziri mkuu Haider al-Abadi.

Mgogoro huo juu ya uchaguzi wa nchini Irak, unaweza kuongeza muda wa mchakato wa kuunda serikali mpya.

Mwandishi: Zainab Aziz/RTRE/APE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga