IOM: Zaidi ya watu 40,000 wakimbia machafuko Port-au-Prince
26 Novemba 2024Shirika linaloshughulikia masuala ya uhamiaji la Umoja wa Mataifa IOM, limesema zaidi ya watu 40,000 wameyakimbia makazi yao katika mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince, katika kipindi cha siku kama kumi hivi mwezi huu, huku mji huo ukikabiliwa na ongezeko la machafuko na uhalifu unaofanywa na magenge.
Shirika hilo limeieleza hali hiyo kama wimbi baya kabisa la watu kulazimika kuyakimbia makazi yao kuwahi kushuhudiwa katika kipindi cha miaka miwili, huku jumla ya watu 40, 965 mjini Port-au-Prince wakiishi mbali na nyumba zao kati ya Novemba 11 na 20, wengine kwa mara ya pili au ya tatu.
Mkuu wa shirika la IOM nchini Haiti Gregoire Goodstein amesema wimbi hili halikutarajiwa tangu walipoanza kushughulikia migogoro ya kibinadamu mnamo 2022. Amesema mgogoro huo ni changamoto ya kibinadamu na mtihani kwa uwajibikaji wao wa pamoja.