1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Inter Milan ni mabingwa wapya wa Ulaya

24 Mei 2010

Van Gaal kocha wa Bayern Munich akubali kushindwa.

https://p.dw.com/p/NVpc
Inter Milan na Kombe laoPicha: AP

Ushindi wa mabao 2:0 wa Inter Milan dhidi ya Bayern Munich,Jumamosi ilioipatia katika Kombe la champions League, mjini Madrid, utakubumkwa kwa mabao 2 maridadi ya muargentina Diego Milito na kocha wa Argentina, Diego Maradona adai ndio maana akamchagua katika kikosi chake cha Kombe lijalo la dunia.

-Bayern, ikiklubali iilizidiwa nguvu na Inter na mbinu za Jose Mourinho, inaangalia mbele ikitumai kuvaa taji lake la 5 la ulaya uwanjani mwake Allianz Arena,2012.

Kinyan'ganyiro cha Kombe la Afrika Mashariki na Kati cha klabu bingwa kinaendelea mjini Kigali, Rwanda bila ya klabu bingwa ya afrika TP mazembe. -nani ataibuika mwishoni mabingwa ?

Na Twiga Stars, timu ya wanawake ya Tanzania inaota ndoto ya kwenda Afrika kusini kwa kombe la Afrika la wanawake.

Diego Milito,ndie aliepiga misumari 2 Jumamosi usiku katika jeneza la Bayern Munich na kuizika kaburini mjini Madrid.

Milito, ni mmoja tu katika waargentina 6 waliotamba katika Champions League msimu huu. Wengine, ni stadi wa barcelona, Lionel Messi,Carlos Tevez,Sergio Aguero na Demichellis wa Bayern Munich.

Baada ya kuitawaza Inter Milan, mabingwa kama alivyoitawaza hapo kabla FC Porto ya Ureno, mabingwa wa champions League, Jose Mourinho, alitangaza kwamba hataendelea msimu ujao kuwa kocha wa Inter Milan,bali atarudi Madrid kuwa kocha wa mabingwa mara kadhaa wa Ulaya,Real Madrid akiongoza kikosi cha akina Christiano Rolando wa Ureno na Kaka wa Brazil.

Mourinho, aliwahi kuwa msaidizi wa kocha wa Bayern Munich huko FC Barcelona.Jumamosi, mwanafunzi alimsomesha darasa la dimba mwalimu wake.Mourinho, baada ya firimbi ya mwisho alimkubatia stadi wa Bayern munich,Arjen Robben,kwani walikuwa pamoja kwa miaka 3 wakati akiichezea Chelsea,mabingwa wapya wa Uingereza.

Lucio wa Brazil, ambae pia alikuwa beki-mshahara wa Bayern Munich, yeye baada ya kulia machozi kwa ushindi ,akiongea na wenzake wa zamani katika Bayern Munich.

Kocha Van Gaal wa B.Munich waliamkiana kirafiki kabisa hata kabla firimbi ya mwisho kulia.Van Gaal baada ya ushindi wa Inter alisema,

"Tunabidi kuwa tumejiandaa barabara ili kuweza kuishinda timu kama Inter Milan.Pia kushambulia ni taabu zaidi kuliko kujilinda."

Van Gaal , akibainisha kwamba timu yake ilianguka mateka wa hujuma zake pale mkorofi Milito, alipotoboa tundu katika ngome yao.

Wakati Diego Maradona, akiwashangiria waargentina wake waliotamba katika Champions League, Dunga, kocha wa Brazi, hatumai mastadi wake 3 waliotamba juzi Jumamosi na Inter Milan, hawatajiunga na kikosi cha Taifa hadi Alhamisi hii ijayo kwa maandalio ya kombe la dunia.

Mastadi hao ni kipa Julio Cesar , mabeki- mshahara Maicon na Lucio.Alhamisi hii ijayo, mastadi hao lakini watawasili johannesberg kujiunga na kambi ya Brazil.

Brazil wako kundi moja na Ivory Coast,Ureno na Korea ya kaskazini.

Mpango wa Korea ya kaskazini wa kupiga kambi nchini Zimbabwe, jirani na Afrika Kusini kujiandaa kwa Kombe la dunia umefutwa kutokana na vitisho hasa huko Matabeleland.

Kikosi cha Korea ya kaskazini , kilikuwa kiwasili kesho ,lakini, wafuasi wa chama cha MDC cha waziri-mkuu Tsavingrai,wanapinga ziara hiyo nchini mwao.Itakumbukwa kuwa, Jeshi la Korea ya Kaskazini,1983, ndilo lililotoa mafunzo kwa Jeshi Jipya la Zimbabwe ambalo latuhuimiwa kuhusika katika kuuwawa kwa maalfu ya raia hasa huko Matabeleland.

Kinyan'ganyiro cha Kombe la klabu bingwa -kanda ya Afrika Mashariki na kati kinaendelea mjini Kigali,Rwanda kuania Kagame Cup.Mabingwa wa Afrika TP Mazembe wametimuliwa nje ya mashindano hayo kwa kumpiga rifu wakati wa mpambano na wenyeji.TP mazembe, huenda isialikwe tena kushiriki katika mashindano haya.

Twiga Stars, timu ya Taifa ya wasichana ya Tanzania, ilijaza kikapu kitupu cha Waeritrea mwishoni mwa wiki kwa mabao 8-1 na kufungua mlango wazi wa kushiriki katika Kombe la Afrika la wanawake nchini Afrika kusini mara tu Kombe la Dunia limemalizika: Duru ya pili itakuwa Eritrea na watanzania watapaswa kujirekebisha na hali ya hewa ya baridi huko.

Mwandishi: Ramadhan Ali/RTRE

Imepitiwa na:Hamidou Oummilkheir