1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Intaneti yarejea Somalia baada ya wiki tatu

17 Julai 2017

Huduma za mtandao wa intaneti zimerejea nchini Somalia baada ya kukatika kwa zaidi ya wiki tatu na kuigharimu nchi hiyo ya Pembe ya Afrika kiasi cha dola milioni 10 kwa siku, wamesema maafisa nchini humo.

https://p.dw.com/p/2ggHu
Journalistentraining in Somaliland Juli 2017
Wanafunzi wa kozi ya uandishi habari wakirambaza kwenye mtandao.Picha: DW Akademie/H. Weithöner

Hormuud Telecom, kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano nchini Somalia, ilitangaza kurejeshwa kwa huduma ya mawasiliano kupitia ujumbe mfupi kwa wateja wake. Kukatika kwa huduma za intaneti kulisababisha ghadhabu nchini Somalia kote na kuathiri maeneo ya kati na kusini mwa nchi, ukiwemo mji mkuu Mogadishu.

Serikali iliutaja ukatikaji huo kuwa ni janga kubwa. Maafisa na watoaji wa huduma za intaneti wamesema tatizo hilo lilisababishwa na meli ya kibiashara iliyokata kebo ya chini ya bahari.

Makampuni makubwa yameripoti hasara ya mapato inayofikia mamilioni ya dola. Shughuli za vyuo vikuu zilivurugwa pia na ukatikaji huu wa huduma ya intaneti. Pia ulitatiza juhudi za kukabiliana na ukame uliolikumba taifa zima na kuwafanya kiasi nusu ya raia milioni 12 wa taifa hilo kuhitaji msaada wa chakula.

Symbolbild  Cyberattacke Virus Wurm Virusattacke
Kukatika kwa huduma za intaneti kumevuruga shughuli nyingi nchini Somalia na kusababisha hasira miongoni mwa watumiaji.Picha: picture alliance/dpa

Wakaazi wa mji mkuu walisherehekea kurudi kwa huduma hiyo. "Hii ni habari njema kweli. Tumekabiliwa na wiki kadhaa za kukatika kwa huduma ambazo zimeathiri biashara zetu vibaya sana," alisema Ahmed Mohamed, meneja wa kampuni ya usafiri ambayo ililaazimika kufunga shughuli zake wakati wote huduma hiyo ilipokuwa haipatikani.

Ukosefu wa huduma za intaneti uliwakwamisha pia wagonjwa waliokuwa wanatafuta matibabu nje ya nchi kutokana na kushindwa kukamilisha nyaraka za mtandaoni. "Baba yangu alikwama Mogadishu kutokana na kukatika kwa mtandao. Sasa tunaweza kumpeleka India baada ya kupokea nyaraka zote za kitabibu kupitia mtandaoni," alisema Nur Hussein.

Somalia inajaribu kujitoa katika mgogoro wa robo karne. Serikali kuu dhaifu inaendelea kuwa shabaha ya kundi la itikadi kali lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda la Al-Shabaab, ambalo mara nyingi hufanya mashambulizi hatari katika mji mkuu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Ape

Mhariri: Josephat Charo