1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Infantino: Mizozo ikome wakati wa kombe la dunia

Josephat Charo
15 Novemba 2022

Rais wa shirikisho la soka ulimwenuni FIFA Gianni Infantino ameitaka Urusi na Ukraine zikubaliane na zisitishe mapigano kwa mwezi mmoja wakati wa mashindano ya kombe la dunia Qatar 2022.

https://p.dw.com/p/4JYek
FIFA Chef Infantino
Picha: Ronald Zak/AP/picture alliance

Infantino ameuambia mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi zilizostawi na zinazokua kwa kasi kiuchumi duniani za G20 nchini Indonesia kwamba kombe la dunia linatoa jukwaa maalumu la amani na umoja kwa sababu mashidano hao yataangaliwa na watu kiasi bilioni tano kupitia televisheni.

"Soka na kombe la dunia la kandanda linawapa ninyi viongozi na dunia jukwaa muhimu na maalum la umoja na amani kote ulimwenguni. Kwa hivyo tuichukue fursa hii tufanye kila tunaloweza kuanza kufikisha kikomo mizozo yote."

Katika hotuba yake rais huyo wa FIFA ametambua hali ya wasiwasi inayoshuhudiwa ulimwenguni wakati huu na kuzitambua nchi zinazokabiliwa na mizozo. Infantino amesema Urusi iliandaa kombe la dunia 2018 na Ukraine inataka kuyaandaa mashindano hayo 2030, pamoja na Ureno na Uhispania, miongoni mwa nchi nyingine zinazotaka kuyaandaa.

Infantino alikuwa akizungumza siku tano kabla mashindano ya 22 ya kombe la dunia la FIFA kuanza Qatar, na siku moja baada ya shirikisho hilo kuzindua kampeni mahususi iliyopewa jina Football Unites the World - Soka linaunganisha Dunia, ambapo wachezaji kadhaa nyota walijumuika pamoja kusisitiza uwezo mkubwa wa kandanda usiopingika, kuwaleta watu pamoja. Kampeni hiyo itaendelea wakati wote wa michuano ya kombe la dunia.

Fußball Nationalspieler | Lionel Messi Argentinien
Lionel MessiPicha: John Walton/PA/picture alliance

Mesi kuiongoza Argentina Qatar

Wakati hayo yakiarifiwa nyota wa Argentina Lionel Messi amesema ana uangalifu kuhusu fursa za Argentina katika kombe la dunia, wakati anapojiandaa kwa michunao hiyo huku akipania kushinda taji ambalo mpaka sasa hajafanikiwa kulipata katika maisha yake ya kutandaza kandanda. Messi amesema Brazil, Ufaransa na England ndizo timu kali na kitisho kikubwa kwa ndoto yao ya kushinda kombe la dunia Qatar. Mshambuliaji huyo wa klabu ya Paris Saint Germain kwa mara nyingine tena atayabeba matumaini ya Argentina nchini Qatar wakati watakapojaribu kushinda kombe la tatu na la kwanza tangu kombe la dunia la 1986.

Kwa upande mwingine rais wa Liberia George Weah anapanga kwenda Qatar kumtazama mtoto wake Tim Weah, akiichezea Marekani katika kombe la dunia. Weah mwenyewe hakufanikiwa kucheza katika kombe la dunia licha ya kuwa miongoni mwa majina makubwa katika ulimwengu wa soka. Anatarajiwa kuwasili Qatar leo Jumanne na atakaa huko kwa siku tisa na kuwa na fursa ya kutazama kipute kati ya Marekani na Wales Jumatatu Novemba 21 katika mechi ya kundi B.

Michuano ya kombe la dunia inaanza Jumapili Novemba 20, wakati Qatar ina miadi na Ecuador katika uwanja a Al Bayt. Mashindano hayo yatakamilika Desemba 18 kwa mechi ya fainali itakayochezwa katika dimba la Lusail.

(afp, reuters)