Indonesia yaomba msaada wa dharura wa kimataifa
1 Oktoba 2018Rais Joko Widodo ameiamuru idara ya majanga na msaada wa dharura kukubali misaada itakayotolewa na mashirika ya misaada pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yako tayari kutoa msaada wa uokozi.
Umoja wa Ulaya umesema umetoa msaada wa dharura wa kibinaadamu wa Euro milioni 1.5, huku Marekani ikisema kuwa iko tayari kutoa msaada wa uokozi. Rais Widodo amesema serikali yake inafanya juhudi za kupata chakula zaidi pamoja na mafuta haraka iwezekanavyo.
Chakula kusambazwa
''Leo tutapeleka chakula kingi tuwezavyo kwa kutumia ndege, moja kwa moja kutoka Jakarta, Balikpapan na Makassar. Haya ndiyo matatizo tunayojaribu kuyatatua kwa sasa pia. Tunatarajia kupata mafuta kutoka Palu, kwa sababu ndege maalum zimepelekwa huko ili kuwaokoa watu,'' amesema Widodo.
Mkurugenzi mkuu wa shughuli za dharura katika idara ya majanga ya kimataifa na uokozi, Nugroho Budi Wiryanto, amesema kukosekana kwa vifaa muhimu vya uokozi pamoja na mafuta, kunaifanya shughuli hiyo kuwa ngumu.
Amesema wafanyakazi wa uokozi walisafiri jana mchana hadi kwenye wilaya ya Donggala kwa kutumia boti na hadi sasa wamefanikiwa kuzipata maiti nane. Waokoaji wanakabiliwa na upungufu wa vifaa wakati wanajaribu kuwafikia waathirika waliokwama katika vifusi vya majengo yaliyoporomoka.
Kwa mujibu wa idara ya uratibu wa majanga ya Indonesia, idadi ya waliokufa kutokana na matetemeko hayo ya ardhi na tsunami iliyokikumba kisiwa cha Sulawesi Ijumaa iliyopita, imefikia 844, ingawa maafisa wameonya kuwa idadi hiyo inaweza ikaongezeka. Aidha, watu wengine 48,000 hawana makaazi kutokana na majanga hayo.
Hayo yanajiri wakati ambapo watu wanaojitolea nchini Indonesa wameanza kuizika miili ya watu waliofariki katika kaburi moja. Kaburi hilo la pamoja litakuwa na uwezo wa kuwazika zaidi ya watu elfu moja. Imeelezwa kuwa kuna baadhi ya maeneo ambayo hadi sasa hayajaweza kufikiwa, huku dawa zikiwa zinakaribia kumalizika.
Matetemeko hayo yametokea baada ya zaidi ya watu 550 kufa na wengine zaidi ya 400,000 kuachwa bila makaazi mwezi Agosti kutokana na mfululizo wa matetemeko ya ardhi kwenye kisiwa cha Lombok, Indonesia.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, DPA, Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman