India yakasirishwa kitendo cha kudhalilishwa kwa mwanadiplomasia
19 Desemba 2013India imekieleza kitendo hicho, kufungwa pingu na kupekuliwa kwa kuvuliwa nguo kuwa cha kikatili na kuchukiza.
Mwanadiplomasia huyo alikamatwa na kufungwa pingu kwa tuhuma za kuwasilisha nyaraka bandia ili kupata kibali cha kazi kwa ajili ya mfanyakazi wake wa nyumbani mjini Manhattan.
Akielezea tukio hulo na kunukuliwa na vyombo vya habari, mwanadiplomasia huyo ambaye ni naibu afisa mkuu wa ubalozi mdogo wa India mjini New York, Devyani Khobragade amesema alilia sana kwa kitendo cha kuvunjiwa heshima kwa kuvuliwa nguo na kufungwa huku akishikiliwa kwa kuchanganywa na watuhumiwa wengine wa makosa ya jinai na matumizi ya madawa ya kulevya.
Anasema na hapa alipata nguvu na kutuliza akili
na kufikiria utu zaidi huku akiwaza jambo moja kwamba ni lazima awawawakilisha watu wake na nchi yake kwa jumla kwa kujiamini na kwa ujasiri.
Kufuatia kitendo hicho, msemaji wa Wizara ya nje wa Marekani, Marie Harf amekilaani kitendo hicho kuwa ni cha ubaguzi na kitengo chake kimelichukulia suala hilo kwa umuhimu mkubwa na kulifanyia kazi kutathimini namna kitendo hicho kilivyotokea.
Maafisa wa India waliondoa vizuizi kwa usalama kwenye barabara ya kuelekea Ubalozi wa Marekani mjini New Delhi , katika kile kilichoelezwa kuwa ni kulipiza kisasa.
waandamanaji wataka Marekani iombe radhi
Huko India, makundi madogo madogo ya waandamanaji yalikusanyika nje ya Ubalozi wa Marekani mjini New Delhi, wakiwa wameshikilia mabango yenye ujumbe kuwa Marekani lazima ibadili mwelekao wake dhidi ya raia wa India na wengine wakipiga kelele wakiitaka Marekani kuomba radhi.
chama cha siasa kali za kizalendo Shiv Sena nacho kiliandaa mandamano ya kuipinga Marekani leo, huku washiriki wakipiga kelele kumlaani rais Barack Obama.
Mwanadiplomasia huyo alikamatwa wakati alipompeleka shuleni mtoto wake wa kike,na aliwekwa ndani kabla ya kuachiwa kwa dhamana ya dola 250,000.
Kiongozi mmoja wa chama cha upinzani nchini India, Bharatiya Janata-BJP- amelaani kitendo hicho akisema hakikubaliki katika jamii.
Kiongozi mwingine amesema hicho ni kinyume cha makubaliano ya mikataba ya kimataifa, hasa ikizingatiwa kwamba wakati raia wa Marekani wanapoitembelea India, hupewa heshima zote.
Mwandishi: Flora Nzema/DPAE
Mahariri: Mohammed Abdul/Rahman