1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

India yaanza kupokea shehena ya vifaa tiba

Sylvia Mwehozi
27 Aprili 2021

India imeanza kupokea vifaa tiba muhimu kutoka nchi mbalimbali wakati ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona yakisababisha idadi ya vifo kufikia 200,000.

https://p.dw.com/p/3seCA
TABLEAU | Coronavirus Indien
Picha: High Commission of India for Singapore/REUTERS

Shehena ya vifaa kutoka Uingereza zikiwemo mashine 100 za kupumulia na vifaa 95 vya Oksjeni viliwasili mjini Delhi, wakati Ufaransa nayo ikituma vifaa vya oksijeni ambayo vinaweza kuwahudumia wagonjwa 250. Waziri wa mambo ya nje wa Uhispania Arancha Gonzalez Laya amesema nchi yake itapeleka tani saba za vifaa tiba kwa India ili kuisaidia nchi hiyo kukabiliana na wimbi la pili la Covid-19.

"Hakuna atakayekuwa salama hadi pale sote tutakapokuwa salama", alisema waziri huyo alipozungumza na waandishi wa habari Jumanne.Hali ya maambukizi imekuwa mbaya nchini India

Mkuu wa kituo cha majeraha ya uti wa mgongo cha India Dkt. K Preetham, anasema "Kwa siku saba, wengi wetu hatukalala" akiongeza kwamba uhaba wa Oksijeni ulikuwa wa mashaka makubwa. Amelieleza shirika la habari la Reuters kwamba uhaba huo ulichangia wagonjwa wawili kuwekwa kwenye kifaa kimoja.

Shirika la afya ulimwenguni WHO limesema kwamba linafanya kazi ili kupeleka vifaa 4,000 vya oksijeni ndini India, ambako "kimbunga" cha mikusanyiko mikubwa, aina mpya zaidi ya virusi vipya na kiwango duni cha utoaji chanjo vimechangia mlipuko huo. WHO imesema kwamba watu nchini humo wamekuwa wakikimbilia hospitali pasi na ulazima, na hivyo kuzidisha hofu.

TABLEAU | Coronavirus Indien
Wahudumu wa afya wakiwahudmia wagonjwa New DelhiPicha: Naveen Sharma/ZUMAPRESS/picture alliance

India imezigeuza hoteli na mabehewa ya treni kuwa vituo vya kuwahudumia wagonjwa ili kufidia uhaba wa kukosekana vitanda lakini wataalamu wanasema mgogoro unaofuta unaweza kuwa ukosefu wa wahadumu wa afya. "Kwa bahati mbaya vitanda havitibu wagonjwa, ni madaktari na wauguzi", anasema Devi Shetty, daktari na mwenyekiti wa hospitali za Narayana.

Chama cha madaktari cha India, kinasema hospitali binafsi kwenye mji wa magharibi wa Surat, zitapaswa kufungwa ikiwa hazitopata vifaa vya oksijeni hivi karibuni.

Ubelgiji imekuwa nchi ya hivi karibuni kuzuia safari za kutoka India, Brazil na Afrika Kusini, mataifa makuu ambayo yameathiriwa vibaya na corona. Zuio hilo linawahusu abiria wote wanaowasili kwa njia ya anga, boti, treni na mabasi, alisema waziri mkuu Alexande de Croo.

Idadi ya vifo visivyorekodiwa

Vifo visivyopungua 1,150 vinavyohusiana na Covid-19 havijajumuishwa katika takwimu rasmi za vifo vya mjini New Delhi, na kuashiria kwamba idadi halisi ya vifo nchini humo kutokana na janga hilo inaweza kuwa kubwa zaidi, kulingana na uchunguzi uliochapishwa Jumanne.

Picha za angani zinazoonyesha idadi kubwa ya miili ikichomwa katika mji mkuu zimeibua wasiwasi juu ya idadi halisi ya vifo inayotolewa na serikali. Uchunguzi huru uliofanywa na kituo cha NDTV kilichoyatembelea maeneo ya kuchoma miili, kimegundua kwamba mamia ya vifo vinavyohusiana na ugonjwa huo havijaorodheshwa kwenye takwimu rasmi.