India yavunja rekodi
15 Februari 2017Kwa mujibu wa kitabu cha kumbukumbu cha Guiness, wimbo huo uitwao "Jana Gana Mana" uliimbwa na watu 509,261 mjini Gujarat, ambako ndiko anakotokea Waziri Mkuu Narendra Modi, wakati wa uzinduzi wa hekalu moja la Kihindu.
Wafuatiliaji mambo wanasema tukio hilo liliwavutia watu wapatao milioni moja, lakini ni nusu yao tu walioweza kuingia kwenye eneo hilo. Ingawa sherehe hiyo ilifanyika mwezi Januari, imeweza kuingizwa rasmi kwenye kitabu hicho cha kumbukumbu leo.
Mkusanyiko huu unavunja rikodi iliyowekwa na Bangladesh mwaka 2014, ambapo watu 254,000 walikutana kwenye mji mkuu wa nchi hiyo, Dhaka.
"Tunaona fahari kubwa kuweza kuweka rikodi hii, ambayo ni zaidi ya mara mbili ya rikodi ya mwisho," alisema Paresh Gajera, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya sherehe hiyo.
Juhudi hizi za kujenga moyo wa utaifa zinakuja huku kukiwa na mjadala mkali juu ya namna wimbo huo wa taifa unavyotumiwa na serikali ya Modi kujenga taswira ya ukandamizaji dhidi ya wengine.
Mnamo mwezi Novemba, Mahakama ya Juu iliamua kwamba majengo yote ya sinema yanapaswa kuonesha wimbo wa taifa kabla ya filamu kuanza na watazamaji wanapaswa kusimama kwa heshima ya wimbo huo, uamuzi ambao ulizua hasira kubwa kutoka kwa watetezi wa haki za kiraia.
Kumekuwa na taarifa za watazamaji sinema kushambuliwa kwa kukataa kusimama, huku wengine wakikamatwa kwa kutoheshimu uamuzi huo wa mahakama.
Wakosoaji wanasema uhuru wa kujieleza unakandamizwa na chama cha Bharatiya Janata cha Modi kilichoingia madarakani mwaka 2014.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman