1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waandamanaji wauawa nchini India

Zainab Aziz Mhariri: Rashid Chilumba
22 Desemba 2019

Waandamaji wauawa nchini India wakati waziri mkuu Nerendra Modi akikutana na wabunge kujadili mswada juu ya sheria ya uraia ambayo waislamu wanasema inawabagua.

https://p.dw.com/p/3VDhN
Indien neues Staatsbürgerschaftsrecht Proteste
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Das

Maelfu ya watu wamejiunga na wimbi jipya la maandamano dhidi ya sheria mpya ya uraia nchini India huku idadi ya waliokufa katika vurugu hizo za karibu wiki mbili ikifikia watu 23. Kwa mujibu wa taarifa watu haowapatao 23 wamekufa kutokana na harakati za kuupinga mswada huo na hakuna dalili za kuonyesha kuwa harakati hizo zitafikia mwisho karibuni.

Waziri mkuu Modi alikutana na mawaziri wake hapo siku ya Jumamosi wakati ambapo vitendo vya kutumia nguvu vikiendelea dhidi ya wapinzani wa mswada huo. Waandamanaji mara kadhaa wamepambana na polisi. Watu wengine watano walikufa kwenye jimbo la Uttar Pradesh wakati waziri mkuu Modi alipokuwa anakutana na baraza lake la mawaziri. Waandamanaji wannne walikufa kutokana na majeraha ya risasi baada ya polisi kuanza kutumia nguvu.

Mswada huo ni juu ya kuibadilisha  sheria itakayowawezesha watu wa jamii za wachache kutoka nchi nyingine kupewa uraia nchini India lakini waislamu hawatapewa haki hiyo. Kulingana na mabadiliko ya  sheria hiyo, itakuwa rahisi kwa watu wa jamii za wachache kutoka Bangladesh, Afghanistan na Pakistan kupata uraia wa India lakini sheria hiyo inawabagua wahamiaji wa kiislamu.

Hadi sasa serikali ya waziri mkuu Modi imechukua msimamo mkali dhidi ya wapinzani wa mswada huo. Waziri mkuu Modi wa chama cha wazalendo wa kihindu BJP amekuwa anautetea msimamo wake. Serikali  ya Modi imerejesha sheria ya enzi ya ukoloni inayopiga marufuku mikutano ya watu wanne au zaidi.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi
Waziri Mkuu wa India Narendra ModiPicha: picture-alliance/AP Photo/M. Wyke

Katika hatua ya kukandamiza uhuru wa kutoa maoni, mawasiliano kwa njia ya internet yalikatizwa mara kwa mara kwenye majimbo kadhaa na wizara ya habari na utangazaji ya India imevitaka vyombo vya habari kutotangaza au kuchapisha maudhui yoyote yanayoweza kuchochea ghasia. Serikali ya India imezuia huduma za intaneti zaidi ya mara 100 lakini hatua hizo za serikali hazikufanikiwa kuzuia harakati za waandamanaji.

Waziri mkuu wa Malaysia Mahathir Mohamed ameikosoa sheria hiyo. Mahathir amesema India ni nchi inayofuata sera ya kutenganisha dini na dola na kwamba dini za watu hazipaswi kuwa kipingamizi katika kuomba uraia.

Umoja wa Mataifa umesema marekebisho ya sheria juu ya uraia inawapa kipaumbele Wahindu, Singasinga, Wabuddhisti na jamii nyingine za wachache lakini inawabagua Waislamu. Msemaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa anayeshughulikia masuala ya haki za binadamu Jeremy Laurence ameeleza kuwa Umoja wa Mataifa umeingiwa wasi wasi kwamba sheria hiyo mpya ni ya kibaguzi.

Amesema Umoja wa Mataifa unakaribisha lengo la kuwalinda watu wanaoandamwa lakini amesema sheria hiyo mpya haiwapi haki waislamu. Msemaji huyo ameeleza kuwa sheria hiyo inakwenda kinyume na msimamo wa India wa kuwapa watu wote haki kwa mujibu wa katiba ya nchi. Bunge la India liliipitisha sheria hiyo ya utatanishi wiki iliyopita na kusababisha maandamano makubwa katika sehemu mbalimbali za nchi hiyo. 

Vyanzo:/AP/RTRE