1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

India kuimarisha mahusiano ya kibiashara na Iran

3 Desemba 2013

Serikali ya India inapeleka kikosi cha wahandisi nchini Iran kusaidia kuharakisha kazi ya ujenzi ya kuongeza ukubwa wa bandari ya Chabahar, itakayo hudumia eneo la Asia ya kati mpaka Afghanistan.

https://p.dw.com/p/1AQn0
Eneo la bandari ya Chadahar Iran
Eneo la bandari ya Chahadar IranPicha: picture-alliance/dpa

Bandari hiyo inategemewa kuboresha uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na nchi za Magharibi mwa Asia.

Bandari ya Chabahar iliyopo kusini-mashariki mwa Iran, itaiwezesha India kufungua milango ya kibiashara na Afghanistan ambayo kwa muda imekuwa na vizuizi vya kibiashara, na pia itaendeleza uhusiano wao wa kiusalama, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha India kuikwepa Pakistan kwa kutotegemea njia ya kupitia huko, kutokana na tofauti zao za kisiasa za muda mrefu.

Mradi wa ujenzi wa Kupanua bandari ya Chabahar ulianza muda mrefu ambapo serikali ya India imekuwa ikiufadhili kwa kiwango kikubwa, lakini ulianza kusuasua baada ya Iran kuwekewa vikwazo vya kiuchumi, vilivyoshinikizwa na marekani pamoja na nchi za magharibi wakiitaka nchi hiyo iache mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia, ambapo hivi karibuni nchi hiyo imepunguziwa vizuizi, hali ambayo imefanya India kutumia nafasi hiyo kujidhatiti kibiashara kwa kugharimia kiasi cha dola za kimarekani milioni 100 kwa ujenzi wa Bandari hiyo nchini Iran, na tayari ilikwisha toa kiasi cha dola milioni 100 kwa ujenzi wa barabara yenye umbali wa kilomita 220 kutoka magharibi mwa Afghanistan na kuunganishwa na barabara iendayo katika bandari hiyo ya Chabahar.

Mara tu baada ya mataifa makuu sita Duniani kusaini makubaliano ya kuipunguzia Iran vikwazo, Waziri wa mambo ya kigeni wa India, Sujatha Singh amekutana na naibu waziri wa mambo ya nje wa Iran Ebrahim Rahimpour ili kuweka sawa mikakati ya kujiimarishia hali ya uchumi wa kibiashara katika eneo lao kwa kuharakisha ujenzi wa bandari hiyo itakayowarahisishia shughuli za kibiashara.

Wanawake wa Iran katika biashara India
Wanawake wa Iran katika biashara IndiaPicha: ISNA

Chabahar ni bandari ya kwanza ya nje ambayo serikali ya India imejihusisha moja kwa moja katika kuifadhili ujenzi wake. India pia inafanya jitihada za kukarabati bandari zake za ndani na kuzifanya ziwe za kisasa.nchi nyingine katika eneo la Asia inayojihusisha na ufadhili wa kifedha katika kuboresha bandari za ukanda huo kwa nia ya kuimarisha mfumo wa kiuchumi na biashara ni China, Mpaka sasa nayo imeshafadhili ujenzi wa bandari ya Gwadar na Hambantota huko Sri-Lanka.

Bandari ya Chabahar kwa sasa ina uwezo wa kupokea meli zenye mizigo ya tani milioni 2.5 kwa mwaka ambapo serikali ya Iran inaipanua kwa lengo la kuchukua meli zenye mizigo ya tani milioni 12.5 kwa mwaka.

Eneo la mji lililopo katika bandari ya Chahadar Iran
Eneo la mji lililopo katika bandari ya Chahadar IranPicha: Behzad Shirzadi

Mpango wa serikali ya India katika ujenzi wa kupanua bandari hiyo, ni pamoja na kukarabati miundo mbinu yote inayozunguka eneo la bandari hiyo,na kuwa na makubaliano ya ubia wa muda mrefu katika uendeshaji wa sgughuli zake.

Hata hivyo mpaka sasa Iran haijazungumza kitu kuhusiana na ubia wa kibiashara katika bandari hiyo na India,ingawaje india imeshajikita kuufadhili mradi wa ujenzi huo,ambapo bado haijajulikana kama uendeshaji wa biashara wa bandari hiyo utakuwa wa manufaa kwa kurudisha gharama walizoingia India kenye ujenzi wake.

Mwandishi: Diana kago/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf