1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF, EU kuipa fedha Ireland

Sekione Kitojo22 Novemba 2010

Umoja wa Ulaya (EU) na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF) zimekubali kuipatia Ireland fedha kwa ajili ya kujikwamua katika matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi hiyo

https://p.dw.com/p/QEvf
Gavana wa Benki Kuu ya Ireland, Patrick Honohan
Gavana wa Benki Kuu ya Ireland, Patrick HonohanPicha: AP

EU pamoja na IMF, kwa pamoja, wataipa Ireland kiasi cha Euro bilioni 80 hadi 90 ili kuiokoa nchi hiyo kutoka hatari ya kuporomoka kiuchumi, imefahamika hapo jana.

Kamishna wa masuala ya uchumi na fedha wa EU, Olli Rehn, amesema kuwa wataalamu kutoka Halmashauri ya umoja huo, Benki Kuu ya EU pamoja na IMF, watatayarisha mpango wa miaka mitatu wa mikopo ifikapo mwishoni mwa mwezi huu.

Waziri Mkuu wa Ireland, Brian Cowen, ametoa baadhi ya maelezo haya katika mkutano na waandishi habari uliofanyika jana (21 Novemba 2010) mjini Dublin.

Gavana wa Benki Kuu ya Ireland, Patrick Honohan, amesema kuwa makubaliano hayo yataruhusu mwelekeo wa sera za kiuchumi na kifedha kuwekwa katika njia iliyo salama.

Jana Jumapili (21 Novemba 2010), Waziri wa Utalii wa Ireland, Mary Hanafin, akizungumza katika televisheni ya RTE, amesema kuwa Ireland itachapisha mpango wake wa miaka minne kwa ajili ya mpango wa Euro bilioni 15 wa hatua za kubana matumizi siku ya Jumatano.

Mwandishi: Sekione Kitojo

Mpitiaji: Hamidou Oummilkheir