1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Imani potofu zaiendeleza Ebola mashariki mwa Kongo

19 Septemba 2018

Licha ya kutangazwa kutokomezwa, bado ugonjwa wa Ebola unaripotiwa kuendelea kuwapo katika maeneo kadhaa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa mujibu wa mwandishi wa DW aliyeko mashariki mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/359IX
Kongo Ebola
Picha: picture-alliance/AP Photo/J. Bompengo

Kundi la madaktari linalokabiliana na ugonjwa wa Ebola mashariki mwa Kongo linaripotiwa kukumbwa na vikwazo vinavyotokana na fikra potofu ya baadhi ya wakaazi wa huko kuwa ugonjwa huo haupo kabisa katika maeneo ya Beni na Butembo. 

Akizungumza na wanahabari mjini Beni, baada ya kuuzuru mji mdogo wa Mangina ambao ndio kitovu cha homa ya Ebola katika eneo hilo, Askofu wa Dayosisi ya Butembo-Beni, Paluku Sikuli Melchissedech, alisema kuwa yeye kama "mchungaji wa kondoo wa Mungu anayezijuwa athari ya homa ya Ebola" ameshapata chanjo dhidi ya Ebola, kwa hiyo anawaomba wakazi wa eneo hili kukubali kupata chanjo hiyo, ikiwa wataalamu wa masuala ya afya wataamua kufanya hivyo. 

Askofu Melchissedech alisema hayo baada ya wakaazi wa eneo hili kufuata matamshi ya mwanasiasa mmoja mashuhuri ambaye anaonekana kuwa bado na mashaka kuhusu chimbuko la Ebola katika eneo hilo.

Upotoshaji wa wanasiasa

"Kama mchaguliwa kama huyo anakuja kuwaambia watu mambo kama hayo, anajisaliti mwenyewe kwani ni wao wanaochapa kazi bungeni! Kwa nini hawakuja kuwanyooshea kidole na kuwataja kwa majina pale wakisema eti walikuweko niliona?", alihoji Askofu Melchissedech akionya kwamba mwanasiasa kama huyo anapaswa kuvuliwa kinga na kutupwa jela.

Infografik Ebola Kongo 2018 EN
Mchoro wa jinsi ugonjwa wa Ebola ulivyoathiri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Hali hiyo ya watu kupinga kuwepo kwa homa ya Ebola katika eneo hilo imepelekea kikundi cha matabibu wanaokabiliana na homa hii kuonekana wakichelewa kuchukuwa hatua za kuukabili ugonjwa huo katika maeneo mbalimbali. 

Ili kuwaunga mkono matabibu katika kuwahamasisha wakaazi wa kata mbalimbali za mji wa Beni,  ikiwa ni pamoja na kutoa chanjo kwa watu walio karibu na walioambukizwa au kufariki kutokana na homa ya Ebola, Naibu Meya wa Mji wa Beni, Bakwanamaha Modeste, alianzisha kampeni ya kuwahamasisha wakaazi kuhusu athari ya homa ya Ebola, kwa kutoa mihadhara.

Watu 111 wameambukizwa na homa ya Ebola katika eneo la mashariki mwa Kongo, ambapo 66 wamepoteza maisha na 38 wameweza kutibiwa.

Mwandishi: John Kanyunyu/DW Beni 
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman