1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ijuwe programu ya SPD endapo ikishinda

Oumilkheir Hamidou
9 Juni 2017

Chama cha Social Democrat (SPD) kinasema kwenye programu yao ya uchaguzi mkuu kuwa kitawapunguzia mzigo waatu wenye mapato madogo na ya wastani, kikitazamia kiongozi wake, Martin Schulz, atachaguliwa kuwa kansela.

https://p.dw.com/p/2eQNb
Deutschland Nach der Landtagswahl in Nordrhein-Westfalen - SPD
Picha: picture-alliance/dpa/K. Nietfeld

Licha ya mapigo matatu yaliyofuatia moja baada ya jengine katika chaguzi tatu za majimbo - chaguzi zilizokuwa zikitajikana kama ishara ya upepo utavuma upande gani katika uchaguzi mkuu wa Septemba, Schulz anashadidia kuwa wamedhamiria kuondoka na ushindi.

"Tumepania kwa moyo ule ule wa ujasiri na ukakamavu. Tunataka kuwa chama chenye nguvu zaidi cha kisiasa katika Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani", anaamini rais huyo wa zamani wa Bunge la Ulaya.

Schulz anataka kuuambatanisha mkakati wake wa kampeni ya uchaguzi na ule uliofuatwa na rais mpya wa Ufaransa, Emmanuel Macron, ili baada ya uchaguzi wapate kukamata usukani wa kuuimarisha Umoja wa Ulaya.

Anasema wakati umewadia wa kuwa na kansela wa Ujerumani ambaye pamoja na rais wa Ufaransa wataanzisha juhudi za kuhakikisha ukuaji wa haki wa kiuchumi barani Ulaya.

Mkuu wa kundi la SPD katika bunge la shirikisho, Thomas Oppermann, anaiitaja programu ya uchaguzi ya chama chake kuwa bora kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu enzi za Willy Brandt. 

"Tumepitisha programu madhubuti kabisa. Ratiba inayodhamiria kuona watu wanaishi katika hali ya usalama nchini Ujerumani, kwamba nchi yetu inafuata mkondo wa kimamboleo na kuhakikisha usawa kwa wote. Huu ni mpango madhubuti. Wananchi wana chaguo bayana kati ya SPD na vyama vya CDU/CSU," anasema Oppermann akielezea namna anavyofurahikia kampeni za uchaguzi wa mwaka huu, kwa sababu zitakuwa kampeni zitakazotuwama katika masuala muhimu.

Suala la haki na usawa katika jamii lapewa umuhimu mkubwa

Deutschland Thomas Oppermann, Fraktionsvorsitzender der SPD
Thomas OppermannPicha: picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka

Oppermann anayaorodhesha masuala hayo kuwa ni pamoja na kwa jinsi gani Wajerumani wanaweza kuiongoza nchi yao katika mustakbali mwema, kwa jinsi gani wataweza kuyashughulikia matatizo yanayowakabili wananchi, kwa jinsi gani wanaweza kusaidia na kwa jinsi gani wanaweza "kuhakikisha usawa na haki kwa wale wanaofanya kazi za sulubu pia."

Katibu Mkuu wa SPD, Katarina Barley, anaichambua programu hiyo kwa kusema kuwa kwayo chama chake kinataka kupigania haki kubwa zaidi.

"Tunaishi katika nchi imara, iliyofanikiwa kiuchumi, lakini dhahiri ni kwamba ufanisi huo wa kiuchumi hauwafikii kwa namna moja wakaazi wote. Tunataka hali hiyo ibadilike na hilo ni dai la tangu jadi la SPD," anasema Barley.

Hapana shaka, mada kuhusu Ulaya na hali ya siku za mbele, sawa na uwekezaji na ubunifu ni miongoni mwa vipaumbele vya SPD pia, na ndio maana, kwa mujibu wa Barley, "Suala hapa sio tu haki na usawa katika jamii, bali tafsiri pana zaidi ya neno haki na usawa."

SPD inasema kuwa jamii inapowekeza, huwa unachangia pia kuleta haki na usawa na hasa kati ya vizazi na, kwa hivyo, Ujerumani "itaweza tu kuendelea kuwa na nguvu kiuchumi ikiwa itutawekeza katika miradi ya utafiti, elimu na miundo mbinu."

Usalama washika nafasi ya juu

Niedersachsens Innenminister Boris Pistorius zu Abschiebungen
Boris PistoriusPicha: picture alliance/dpa/P. Steffen

Mada kuhusu usalama pia inatarajiwa kuhanikiza katika kampeni za uchaguzi, yakitiliwa maanani mashambulizi ya kigaidi ya yaliyoitikisa Ujerumani na kwengineko barani Ulaya.

Hata mjadala kuhusu programu ya uchaguzi ya SPD ulikawia kuanza kufuatia onyo la kutokea mashambulizi katika makao makuu ya chama hicho, katika jengo la Willy Brandt mjini Berlin. Baada ya uchunguzi lakini ikagunduliwa kuwa kifurushi kilichoshukiwa hakikuwa na miripuko.

Usalama ni suala muhimu kwa maisha ya kila raia. SPD wanahisi ni jukumu la serikali kudhamini usalama na hivyo wanataka polisi wengi zaidi wawekwe mitaani, polisi 15.000 zaidi waajiriwe katika daraja ya shirikisho na majimbo na uchunguzi katika mipaka ya nje ya kanda ya Schengen uimarishwe.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa jimbo la Lower Saxony, Boris Pistorius, anahisi baada ya pigo katika chaguzi tatu za majimbo, SPD wanabidi watangulize mbele suala la usalama wa ndani katika kampeni ya uchaguzi mkuu.

Akizungumza na jarida la der Spiegel, Pistorius anasema usalama wa ndani ni mahitaji ya kimsingi ya raia na ndio maana chama chake cha SPD kinabidi kiitumie mada hiyo kupata imani ya wananchi kote nchini na kurejesha imani ya wapiga kura.

Maoni sawa na hayo yanatetewa pia na mkuu wa kundi la SPD katika bunge la Shirikisho Bundestag, Thomas Oppermann, ambaye anaesema anataka kuiona nchi ikiwa salama zaidi. "Ninataka wahalifu watakaopatikana Ujerumani washuhudie makali ya sheria, ingawa sisi wana SPD tunatanguliza mbele hatua za kinga. Tunataka kuepusha balaa la vijana kugeuka kuwa wahalifu, watu wanaojihusisha na mashambulizi au kugeuka kuwa magaidi wa itikadi kali ya dini ya Kiislam."

Programu isiyofafanuliwa

Deutschland SPD Schwesig und Sellering
Manuela Schwesig (kulia)Picha: Reuters/T. Schwarz

Hata hivyo, wakosoaji wanahisi programu hiyo haikufafanuliwa kwa shauku na hakujakuwa na maelezo ya kina kuhusu mada mbili kuu zinazohusiana na malipo ya uzeeni na kodi za mapato.

Kwa namna hiyo, wadadisi wanahisi  wana-SPD wanawaachia CDU/CSU uwanja muhimu na kumtakasia njia Kansela Angela Merkel kuelekea chaguzi mkuu wa Septemba.

Programu hiyo ya SPD inataja lengo lao ni kusawazisha kiwango cha malipo ya uzeeni. Aliyefanya kazi kwa miongo kadhaa anastahiki pia malipo yanayolingana na mchango wake. Hata hivyo majadiliano yangali yanaendelea kuhusu mada hiyo.

Naibu Mwenyekiti wa chama hicho, Manuela Schwesig, ambaye pia ni waziri katika serikali kuu inaoongozwa na Kansela Merkel anasema majadiliano makali yatahusiana na suala la uwekezaji na kodi.

"Tunataka kuwapunmguzia mzigo wananchi kwa kuwapatia fedha zaidi kwa ajili ya elimu na pia kwa kuwapunguzia mzigo wa kodi za mapato. Sisi tunaona uwekezaji na kupunguzwa mzigo wa kodi ni vitu vinavyoambatana. CDU/CSU wanataka zaidi kuwekeza katika kurundika silaha. Sisi tunasema wazi wazi, afadhali kuwekeza katika elimu badala ya kuwekeza katika kurundika silaha."

Mgombea kiti cha ukansela kupitia chama hicho, Martin Schulz, anasema wakipania kwa dhati watafanikiwa

"Tukipania na kudhamiria na kuwa kitu kimoja, hapo tutafanikiwa na kansela mpya wa Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani atakuwa Martin Schulz."

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir
Mhariri: Yusuf Saumu