IEBC yafika nusu ya shughuli ya kujumlisha matokeo
14 Agosti 2022Shughuli hiyo imeandamwa na misukosuko kwenye ukumbi wa Bomas huku mawakala wa muungano wa Azimio la Umoja na Kenya Kwanza wakitupiana lawama. Kufikia sasa madawati ya kuhakiki na kujumlisha kura yameongezwa hadi kufikia 12.
Kwa mara ya kwanza tangu siku ya uchaguzi, mgombea wa urais wa Azimio la Umoja Raila Odinga ameonekana hadharani. Jumapili anahudhuria ibada kwenye Kanisa la Mtakatifu.
Wengine walioongozana na Odinga
Francis mtaani Karen akiongozana na mgombea wake mwenza Martha Karua, kiongozi wa muungano wa vyama vya wafanyakazi, COTU, Francis Atwoli, mwenyekiti wa chama cha KANU Gideon Moi na mbunge mteule wa Langata Phelix Kodhe maarufu kama Jalas. Raila Odinga amewarai Wakenya kudumisha amani kama alivyosisitiza Mtakatifu Francis kwenye Biblia.
Kwengineko, gavana mteule wa kaunti ya Nairobi Johnson Sakaja amewashukuru Wakenya na kuahidi kuwa yuko tayari kulinyanyua jiji kuu la Kenya. Akitoa hotuba yake kwenye kituo cha Kasarani cha kuhesabia kura, Johnson Sakaja aliusisitizia umuhimu wa kudumisha amani.
Magavana wote wapya wataapishwa Alhamisi ya kwanza baada ya siku 10 za mshindi kutangazwa rasmi na IEBC. Edwin Sifuna wa ODM ndiye seneta mpya wa kaunti ya Nairobi na amekishukuru chama kwa kumuunga mkono.
Kaunti za Mombasa na Kakamega zinasubiri kuwachagua magavana wao ifikapo tarehe 23 mwezi huu kufuatia changamoto za nyenzo. Ukumbi wa Bomas ulikuwa uwanja wa vita vya maneno usiku wa kuamkia Jumapili.
Pande zote zatupiana lawama
Mawakala wa Azimio la Umoja na wale wa Kenya Kwanza walinyoosheana vidole vya lawama mintarafu karatasi zisizoeleweka. Zogo lilizuka pale wakala wa Raila Odinga wa Azimio la Umoja Saitabao Ole Kanchory aliponyata hadi jukwaani na kudai kuwa uhalifu unafanyika ukumbini. Maafisa wa usalama waliingilia kati na kumtuliza.
Kwa upande wa Kenya Kwanza, Gladys Shollei ambaye ndiye wakala wa William Ruto wa chama UDA alikuwa mstari wa mbele kuwalaumu wapinzani wao akiungwa mkono na Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki na mwenzake wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen.
Kutokana na tukio hilo usalama umeimarishwa kwenye ukumbi wa Bomas na shughuli ya kujumlisha matokeo ikaendelea. Kwa sasa tume ya uchaguzi inaelekea kufikia nusu ya zoezi hilo ukizingatia kuwa maeneo bunge yote ni 290. Madawati ya kuhakiki fomu za 34A yameongezwa hadi 12 ili kuiongeza kasi ya kujumlisha matokeo ya uchaguzi wa rais.