IEBC: Ni vigumu kuhakikisha uchaguzi wa haki
18 Oktoba 2017Siku nane kabla ya kufanyika uchaguzi mpya wa urais hali ya wasiwasi imetanda juu ya iwapo uchaguzi huo utafanyika kwenye mazingira bora na ya kuaminika kama ilivyoamualiwa na mahakama ya Juu. Mwenyekiti wa Tume hiyo Wafula Chebukati ameelezea wasiwasi wake kuhusu mshikamano wa maafisa kwenye Tume hiyo suala ambalo limeigawa tume hiyo na kuliweka taifa katika njiapanda. Chebukati ameeleza kuwa mapendekezo yake yote ya kuhakikisha kuwa uchaguzi unaendeshwa kwa njia huru na ya haki yamekuwa yakipigwa teke na makamishna wenzake.
Upande wa upinzani umekuwa ukishinikiza kuondolewa kwa Afisa mkuu mtendaji wa Tume hiyo Ezra Chiloba na maafisa wengine sita waondoke afisini, hatua ambayo haijatekelezwa. "Katika hali kama hiyo ni vigumu kutoa hakikisho kwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika, Bila ya mageuzi muhimu katika sektariati ya tume uchaguzi huru na wa haki utavurugwa hivyo nawaomba maafisa waliotajwa kavuruga uchaguzi uliopita kungatuka na kuruhusu kikundi nilichobuni kufanya kazi," amesema Chebukati.
Kwenye mkutano na wanahabari Chebukati amesema kuna nafasi ya kunusuru utendaji kazi wa tume hiyo iwapo makamisha wote wataweka tofauti zao kando na kuweka maslahi ya taifa mbele. Huku wengi wakitarajia kuwa angejiuzulu, Chebukati alishikilia kuwa hatajiuzulu. Hata hivyo alikuwa mwepesi wa kusema kuwa hatakuwa sehemu ya kikundi kitakachovuruga uchaguzi ujao kwa manaufaa ya muda mfupi. Amewaonya wanasiasa ambao wanawatisha maafisa wake. "Nawapa wanasiasa wote kadi ya njano, sitaruhusu vitisho kwa maafisa wangu, sitaruhusu kuingiliwa kwa tume yangu tena. Wakenya wanalipa pesa kubwa kugharamia uchaguzi huu. Na kama mwenye wajibu sintoacha pesa za wakenya na washirika wetu zipotee," ameahidi mwenyekiti huyo.
Kenyatta ataka watu waiombee nchi
Akigusia suala la kamishna Roslyn Akombe aliyejiuzulu mapema leo, Chebukati amemtaja Akombe kuwa mmoja wa watumishi wakakamavu waliojitolea kuhudumu kwenye Tume hiyo. Amelaumu tume kwa kushindwa kutoa mazingira yanayostahili kwa kamishna huyo, sababu iliyomfanya ajiuzulu. Wakati huo huo rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto wameendelea na kampeni zao, huku wakiwataka wafuasi wao kujitokeza kwa wingi kurejesha chama cha Jubilee mamlakani kwa kipindi kingine cha miaka mitano. Wawili hao wamesema kuwa hawataruhusu kiongozi wa upinzani Raila Odinga kusitisha mchakato wa uchaguzi mpya wa urais. "Wewe Bwana Odinga kwasababu tumekubali haki ya kukaa nyumbani, kwanini unafikiria kuwa wewe uko na haki ya kukataza wakenya wale ambao wanataka kupiga kura wapige kura, hiyo hatuwezi kukubali," amesema Kenyatta.
Naye Makamu wa Rais William Ruto akaongezea, "Sasa huyu mtu wa vitendawili anasema kuwa atasimamisha uchaguzi, kama Uhuru Kenyatta ambaye ni amiri jeshi mkuu wa majeshi yote ya Kenya, hawezi kusimamisha uchaguzi, sasa mtu wa vitendawili na uganga ataweza, aache mzchezo."
Ili kujikwamua katika mzozo wa sasa, taifa litahitaji vitendo na nia nzuri zaidi ya matamshi kutoka kwa wanasiasa ambao wanavutia upande wao kwani kwa sasa taifa limegawanyika. Mapema Rais Kenyatta aliwataka wakenya wa dini zote kutenga siku ya Jumapili kuombea taifa huku wachambuzi wa masuala ya siasa wakimtaka kuketi meza moja na Odinga kwa mazungumzo.
Mwandishi: Shisia Wasilwa
Mhariri: Iddi Ssessanga