1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IDF yakamata watu 100 kwa shutuma za ugaidi Ukanda wa Gaza

Hawa Bihoga
17 Februari 2024

Jeshi la Israel IDF limesema leo kwamba limewakamata watu 100 wanaoshukiwa kwa shughuli za ugaidi kwenye hospitali ya Nasser iliyopo kwenye mji wa Khan Younis kusini mwa Ukanda wa Gaza.

https://p.dw.com/p/4cWAB
Ukanda wa Gaza | Uharibifu katika hospitali ya Nasser
Uharibifu uliofanywa kwenye hospital ya Nasser kufuatia oparesheni ya Israel.Picha: Mohammed Salem/REUTERS

Vikosi vya IDF viliingia kwenye majengo ya hospital hiyo kwa lengo la kile IDF imesema kuwa ni kukomboa miili ya mateka wa Israel waliokuwa wakishiliwa na Hamas. Hata hivyo jeshi la Israel hadi sasa halijasema iwapo limefanikiwa kuokoa miili ya mateka hao.

Katika taarifa yake jeshi hilo limesema linaendelea na operesheni yake ilioitaja sahihi na yenye mipaka dhidi ya kundi la Hamas ndani ya hospitali hiyo ilioko kusini mwa Gaza.

Kufuatia oparesheni hiyo kumeshuhudiwa madhara kadhaa  ikiwemo wagonjwa 5 katika kitengo cha wagonjwa mahututi kufariki kutokana na kukatika kwa umeme na kukatwa kwa usambazaji wa oksijeni.

Soma pia:Netanyahu apinga kuitambua Palestina kama taifa huru

Wizara ya afya Gaza inayoongozwa na Hamas imesema kwamba wagonjwa wengi wakiwemo watoto wapo hatarini, huku ikishutumu Israel kwa kuzuia kuhamishwa kwa wagonjwa kwenda hospitali nyingine na kuzuia msafara wa Umoja wa Mataifa kuifikia hospital ya Nasser.