Watoto wanaosajiliwa na magenge ya silaha waongezeka Haiti
25 Novemba 2024Shirika linalowahudumia watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF limetahadharisha kwamba idadi ya watoto nchini Haiti waliosajiliwa na magenge yenye silaha imeongezeka kwa asilimia 70 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Shirika hilo limeonya kwamba watoto wanakaribia aslimia 50 ya idadi jumla ya wanachama wa magenge hayo.
Haiti imehangaika kutokana na miongo kadhaa ya kuyumba kwa hali ya kisiasa, lakini katika miezi ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia ongezeko kubwa la machafuko huku magenge sasa yakidhibiti asilimia 80 ya mji mkuu Port-au-Prince.
Katika taarifa yake UNICEF imesema ongezeko hilo ambalo halikutarajiwa, lilirekodiwa robo ya pili ya mwaka 2023 na 2024 na linaashiria mgogoro wa ulinzi wa watoto unaoendelea kuwa mbaya nchini Haiti.