1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya wakimbizi yafikia milioni 40 duniani

Sylvia Mwehozi11 Mei 2016

Idadi ya watu wanaokimbia nchi zao kote ulimwenguni kwa sababu za kivita na vurugu ilifikia milioni 40 kwa mwaka 2015 , huku Yemen ikiweka rekodi ya kuwa taifa lenye wakimbizi wengi wapya

https://p.dw.com/p/1IlYY
Flüchtlinge Grenzgebiet Türkei Syrien
Picha: picture-alliance/dpa/V. Gurgah

Idadi ya watu wanaokimbia nchi zao kote ulimwenguni kwa sababu za kivita na vurugu ilifikia milioni 40 kwa mwaka 2015 , huku Yemen ikiweka rekodi ya kuwa taifa lenye wakimbizi wengi wapya. Ripoti ambayo imetolewa na shirika la kimataifa la misaada inasema kwamba idadi hiyo ya watu inazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na kuzidi kwa vita na machafuko.

Kwa ujumla kumekuwa na kesi mpya za watu milioni 8.6 ambao wamekimbia nchi zao zilizokumbwa na mizozo kwa mwaka jana pekee, ikiwa ni wastani wa watu 24,000 kwa siku. Kituo kinachofuatilia masuala ya watu walioyahama makazi yao, IDMC kimetoa ripoti hiyo ambayo inasema nusu ya hao wametokea Mashariki ya kati.

Watu milioni 2.2 nchini Yemen, sawa na asilimia 9 ya idadi ya watu nchini humo waliyakimbia makazi yao mwaka jana kwa sababu ya vita iliyozuka nchini mwao. Ripoti hiyo inaonyesha , idadi ya watu wanaoyakimbia makazi yao kutokana na vita na mizozo lakini wanabakia nchini mwao ilikuwa ni mara mbili ya wale ambao wamefanikiwa kuingia nchi nyingine wakiwa wakimbizi.

Katibu wa baraza la wakimbizi la nchini Norway ambao ndio waendeshaji wa kituo cha IDMC Jan Egeland anasema na hapa nanukuu, "tunapaswa kutafuta njia za kuwalinda watu kutokana na maafa ya asili na yale yanayosababishwa na mwanadamu", mwisho wa kunukuu.

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia wakimbizi-UNHCR limesema kwamba idadi ya watu ambao wanalazimika kuyakimbia makazi yao ulimwenguni kote ingefikia milioni 60 kwa mwaka 2015, ikuwajumuisha wakimbizi milioni 20 wanaochangiwa na mzozo wa Syria.

Wakimbizi nchini Yemen
Wakimbizi nchini YemenPicha: DW

Ripoti hiyo inasema idadi hiyo ya watu kuyakimbia makazi yao ilichangiwa zaidi na vuguvugu la mageuzi Mashariki ya kati na kaskazini mwa Afrika na kuibuka kwa vita vya kundi linalojiita dola la kiislamu IS katika mataifa ya Syria , Iraq na kwingineko.

Mbali na mizozo hiyo ya kibinadamu, ripoti hiyo pia imeangazia maafa yanayosabishwa na majanga ya asili. Kwa mfano nchini Nepal pekee watu milioni 2.6 walipoteza makazi yao kutokana na tetemeko la ardhi.

Nchi za Cuba, Vietnam na Bangladesh zimefanikiwa katika kuyadhibiti majanga ya asili, huku nchi za Amerika ya Kusini zikiwa bado mkiani katika jitihada za kupambana na maafa.

Katika kilele cha mkutano wa kimataifa kuhusu masuala ya utakaofanyika Instanbul, Uturuki hivi karibuni, ajenda mojawapo itakuwa ni kuzidisha nguvu ya kupambana na majanga ya asili.

Wananchi wakiyakimbia makazi yao Kongo
Wananchi wakiyakimbia makazi yao KongoPicha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Ripoti hiyo inasema "kuongezeka kwa idadi ya wakimbizi kila mwaka" inaonyesha dhahiri kuwa hakuna suluhisho la tatizo hilo.

Colombia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Iraq, Sudan na Sudan Kusini ni miongoni mwa mataifa 10 yaliyo na idadi kubwa ya wakimbizi kila mwaka tangu 2003.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Gakuba Daniel