Idadi ya wagonjwa wa COVID-19 wafikia 94 Tanzania
16 Aprili 2020Wakati huohuo, mamlaka ya mkoa wa Dar es salaam imeanza kusambaza vitakatishaji kwenye mabasi ya daladala huku mamlaka hiyo ikiwaonya abiria wanaokwepa kuvutumia kuwa wataandamwa na mkono wa dola.
Katika taarifa yake kwa umma, Waziri wa afya kisiwani humo, Hamad Rashid Mohamed amesema wagonjwa hao wote ni Watanzania na maambukizi hayo wameyapata wakiwa nchini.
Taarifa ya wagonjwa hao sita inafanya idadi ya wagonjwa visiwani humo kupanda kutoka ile ya awali ya watu 18 hadi kufikia 24.
Taarifa zinasema wagonjwa hao wote sita wamelazwa katika vituo maalumu kwa ajili ya kuendelea na matibabu, huku waziri huyo akirejea wito wa kuwataka wananchi kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo kama zinavotolewa mara kwa mara ikiwemo kunawa mikono na kujiepusha na misongamano.
Wagonjwa 11 tayari wamepona
Taarifa ya wizara ya afya visiwani humo inakuja saa 24 baada ya taifa la Tanzania kutangaza wagonjwa wapya 29 waliokumbwa na virusi hivyo, ambao wengi wao wapo katika jiji la Dar es salaam.
Hadi dakika hii Tanzania ilikuwa na wagonjwa 94 waliokumbwa na janga hilo na kwamba hadi kufikia Jumatano takriban watu 11 walikuwa wameshapona virusi hivyo huku watu wanne wakifariki dunia. Na hadi tunakwenda mitambano upande wa Tanzania bara ilikuwa bado haujatoa taarifa yoyote kuhusu wagonjwa waliothibitishwa kwa siku ya leo.
Wakati huohuo vita dhidi ya maambukizi ya corona vimeimarishwa baada ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kutangaza vituo vya afya na hospitali 25 ambavyo wakaazi watakuwa wakipeleka sampuli zao ili kupimwa virusi vya corona.
Mkuu huyo amesema lengo la vituo hiyo ni kuzuia maambukizi ya virusi hivyo hususan wakati huu ambapo kumekuwepo na ongezeko la wagonjwa. Kama hiyo haitoshi, mabasi ya daladala yanayofanya safari zake ndani ya mkoa wa Dar es salaam yameanza kusambaziwa vitakasa vitakavyotumiwa na abiria wanaotumiwa mabasi hayo.
Wakati huo huo kama sehemu ya kudhibiti kuenenea kwa maambukizi ya virusi hivyo, baadhi ya hospitali kubwa nchini zimeanza kutoa matangazo kuwataka wagonjwa wanaokwenda kutibiwa na wale wanaowatembelea jamaa zao kuhakikisha wanavaa kifaa maalumu cha kujikinga pua na mdomo maarufu kama barakoa.