1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya maambukizi ya corona Tanzania yaongezeka hadi 480

Hawa Bihoga/Dar es salaam29 Aprili 2020

Baada ya kukaa kimya kwa siku kadhaa serikali ya Tanzania imetoka hadharani na kusema visa vya virusi vya corona vimefika 480. Nacho chama cha Chadema kimelishutumu bunge kwa kutoiwajibisha serikali.

https://p.dw.com/p/3bZCf
Tansania Ummy Mwalimu
Picha: picture-alliance/Photoshot

Waziri mkuu Kaasim Majaliwa amesema kuanzia Aprili, 23 hadi 28 2020 wamepatikana wagonjwa wengine wapya wenye maambukizi ya Corona mia moja tisini na sita ambapo kati yao mia moja sabini na nne ni kutoka Tanzania bara na wengine ishirini na mbili ni kutoka upande wa pili wa nchi Zanzibar na hivyo kuwa na jumla ya wagonjwa mia nne themanini.

Taarifa hiyo ya waziri mkuu kwa vyombo vya habari inaonesha kuwa jumla ya waliopona imeongezeka kutoka 48 iliyotangazwa na waziri wa afya juma lililopita hadi kufikia 167 ambapo Zanzibar ni 36 huku bara ikiwa ni 83.

Aidha Waziri mkuu Majaliwa amesema, kuna ongezeko la vifo vya watu sita kutokana na mripuko huo na kufanya jumla ya vifo kuwa 16, huku kati ya wenye maambukizi 297 waliobaki 283 wanaendelea vizuri na 14 wako chini ya uangalizi madhubuti.

Watu wanatakiwa kuvaa barakoa wakiwa katika maeneo ya umma Tanzania
Watu wanatakiwa kuvaa barakoa wakiwa katika maeneo ya umma TanzaniaPicha: DW/S. Khamis

Kabla ya waziri mkuu majaaliwa kutoka hadharani na kutoa maelezo kuhusu hali ya mwenendo wa ugonjwa huo wa covid-19 hii leo baada ya ukimya wa siku kadhaa, video mbalimbali zimekuwa zikisambazwa katika mitandao ya kijamii zikionesha kile kinachodaiwa kuwa ni maiti za watu waliofariki kwa corona, huku zingine zikionesha watu waliovalia mavazi ya kujikinga na maambukizi wakifanya maziko ya waliofariki.

Katika hatua nyingine kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni na mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini chadema Freeman mbowe amelishutumu vikali bunge kushindwa kuisimamia serikali katika utoaji wa taarifa rasmi bungeni kwa ajili ya kuchukuliwa kwa hatua stahiki ikiwemo, utengwaji wa bajeti maalum ambayo itaelekezwa katika mapambano dhidi ya janga la corona nchini.

Kutokana na kuishutumu serikali kwa kile walichokitaja usiri dhidi ya janga la corona, chama hicho kikuu kimeamua kuunda kamati yake ambayo itakuwa na jukumu la kukusanya taarifa zenye ushahidi wa picha na video kuhusu maambukizi ya covid-19 na kutoa taarifa hizo kwa umma pamoja na jumuiya za kimataifa.