ICRC: Libya inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu
16 Septemba 2023Kamati ya kimataifa ya Msalaba Mwekundu ICRC imesema kuwa Libya inakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu iliyosababishwa na mafuriko makubwa na kutoa wito wa msaada zaidi.
Msemaji wa ICRC nchini Libya, Bashir Omar, amesema nchi hiyo inahitaji msaada mkubwa na kwamba mashirika yote ya kimataifa yanayoendesha shughuli zake nchini humo hayana uwezo wa kushughulikia maafa yaliyojitokeza. Umoja wa Mataifa pia umeyataja mafuriko hayo kuwa janga na kutoa wito wa kupatikana kwa zaidi ya dola milioni 71 kuwasaidia waathirika.
Mafuriko yaliyotokea mwishoni mwa Juma lililopita yamesababisha uharibifu mkubwa mashariki mwa Libya haswa katika mji wa bandari wa Derna. Watu wapatao 20,000wanahofiwa kufariki katika mji huo.
Maafisa wa uokozi bado wanaendelea kutafuta manusura zaidi huku maelfu ya watu wakiwa hawajulikani waliko.