1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC: Yumkini Ruto kushtakiwa Afrika

4 Juni 2013

Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu inaweza kuendesha kesi yake kwa mara ya kwanza nje ya The Hague baada ya majaji wake kusema kwamba yumkini wakaendesha kesi dhidi ya makamo wa rais wa Kenya katika nchi yake auTanzania.

https://p.dw.com/p/18jNz
Makamo wa Rais wa Kenya William Ruto.
Makamo wa Rais wa Kenya William Ruto.Picha: dapd

Majaji hao Jumatatu (03.06.2013) walikuwa wakijibu ombi la mawakili wa William Ruto ambao wamesema itakuwa ni kwa "maslahi ya haki" kwa kesi hiyo kusikilizwa mahala palipo karibu na nyumbani.

Ruto pamoja na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya waliochaguliwa kwa kutumia tiketi ya pamoja katika uchaguzi mkuu wa Kenya uliofanyika hapo mwezi wa Machi wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga ghasia za umwagaji damu kufuatia uchaguzi wa miaka mitano iliopita ambapo watu 1,200 walipoteza maisha yao.

Juhudi za kuwashtaki viongozi hao wa mojawapo ya taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Afrika, zinakuja wakati mahakama hiyo ya Kimataifa ya Uhalifu ICC ikiwa inazidi kushutumiwa na viongozi wa Afrika ambao wanaituhumu kwa kuwaandama kusiko haki Waafrika.

Picha ya Uhuru Kenyatta na William Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi wa Kenya mwezi wa Machi 2013.
Picha ya Uhuru Kenyatta na William Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi wa Kenya mwezi wa Machi 2013.Picha: Simon Maina/AFP/Getty Images

Ugumu wa kuendesha kesi nje ya The Hague

Ruto amesema atahudhuria kesi hiyo huko Tha Hague iwapo ataamuriwa kufanya hivyo,lakini pia ameomba kushiriki katika kesi hiyo kupitia kiunganisho cha video.

Juu ya kwamba uamuzi rasmi haukutolewa majaji wa ICC wamesema kuendesha sehemu ya kesi hiyo nchini Kenya au Tanzania ambapo mahakama ya Umoja wa Mataifa inaendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, kutaiweka kesi hiyo karibu na wahanga na jamii zilizoathirika.

Waendesha mashtaka wameonya kwamba kuihamishia kesi hiyo nchini Kenya itakuwa vigumu kuwapatia ulinzi mashahidi ambao wanasema wamekuwa wakitishwa ili wafute ushahidi wao.Kesi hiyo itaendeshwa na ICC mahala popote pale itakaposikilizwa.Mawakili wa Kenyatta wametowa ombi kama hilo la kutaka kesi hiyo ihamishwe.

Majaji pia wameamuwa hapo Jumatatu kwamba kesi ya Ruto na mshtakiwa mwenzake ambaye ni mtangazaji Joshua Arap Sang itaanza kusikilizwa hapo tarehe 10 mwezi wa Septemba badala ya tarehe 28 mwezi wa Mei iliokuwa imepangwa awali kwa kukubali ombi la mawakili wa utetezi la kutaka kupewa muda zaidi wa kujiandaa na kesi hiyo.

Mtangazaji Joshua Arap Sang ambaye pia anakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya ICC.
Mtangazaji Joshua Arap Sang ambaye pia anakabiliwa na mashtaka katika mahakama ya ICC.Picha: picture-alliance/dpa

Kesi tafauti ya Kenyatta ambayo hivi sasa inatazamiwa kuanza kusikilizwa hapo mwezi wa Julai juu ya kwamba mawakili wake wameomba kucheleweshwa na majaji wanatafakari maombi yao.

Watuhumiwa wote hao wamekanusha kuhusika na mashtaka yanayowakabili.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.Picha: Getty Images

Afrika yatuhumu ICC kwa ubaguzi

Viongozi katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika uliofanyika katika makao makuu ya umoja huo mjini Addis Ababa Ethiopia wiki iliopita wameitaka mahakama ya ICC kuzihamisha kesi hizo katika mahakama za Kenya.

Rais wa Ethiopia Hailemariam Desalegn ameishutumu mahakama hiyo kwa kuwa na upendeleo wa kibaguzi na kwa kuwalenga Waafrika kwa ajili ya kuwafungulia mashtaka, madai ambayo daima mahakama hiyo imekuwa ikiyakanusha.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri : Abdul-Rahman,Mohammed