1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yaziomba nchi za Afrika kutojivua uanachama

Caro Robi
16 Novemba 2016

Mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu ya ICC imezitolea wito nchi za Afrika kutojiondoa kutoka mahakama hiyo.Wito umetolewa wakati wa kuanza kwa mkutano wa kila mwaka wa nchi wanachama wa mkataba wa Roma

https://p.dw.com/p/2SmYj
Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag Niederlande
Picha: picture-alliance/dpa/J.Vrijdag

Nchi kadhaa za Afrika katika siku za hivi karibuni zimetangaza zinajiondoa kutoka mahakama ya ICC. Kwanza ilikuwa Burundi, kisha Afrika Kusini na Gambia ikafuata mkondo. Siku ya Jumatatu, wiki hii, Gambia iliifahamisha rasmi Umoja wa Mataifa azma yake ya kujiondoa.

Rais wa ICC Sidiki Kaba, mwanasiasa wa Senegal amewaomba viongozi wa Afrika kutojiondoa ICC akisema katika ulimwengu uliozongwa na ghasia zinazosababishwa na itikadi kali kuna haja ya dharura ya kulinda misingi na haki ya kila mtu.

Kaba amekiri kuwa mahakama ya ICC iliyoanzishwa mwaka 2000 kushughulikia kesi mbaya zaidi za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu inapitia wakati mgumu na kuongeza kuna uchunguzi ulioendeshwa na mahakama hiyo ambao haukuwa wa haki lakini amewahakikishia viongozi kuwa wamesikilizwa.

Viongozi wa Afrika wameishutumu mahakama hiyo kwa kuwaandama na kutoendesha shughuli zake kwa usawa na haki. Kenya, Namibia na Uganda zimedokeza zina nia ya kujiondoa kutoka mkataba wa Roma. Kamishna wa tume ya kutetea haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein amesema licha ya wenye nguvu kutaka kujiondoa kutoka ICC, waathiriwa kwingineko wanaililia mahakama hiyo kuwasaidia.

Niederlande Den Haag Gerichtsvollzieherin Fatou Bensouda beim Fall Jean-Pierre Bemba
Mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Fatou BensoudaPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Lampen

Al Hussein amesema kwa kujiondoa kutoka mkataba wa Roma, viongozi huenda wakajipa kinga lakini kwa gharama ya kuwanyima watu wao ulinzi wa kipekee na kuonya mtindo mpya wa kutaka kujitenga wimbi ambalo limeighubika dunia kwa sasa kutapelekea mashambulizi zaidi dhidi ya mahakama hiyo.

Kati ya kesi kumi zinazoendeshwa na ICC, tisa ni kuhusu nchi za Afrika na iliyosalia inaihusu Georgia. Hapo jana mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya ICC, Fatou Bensouda alisema kuna sababu ya kuanzisha uchunguzi dhidi ya wanajeshi wa Marekani kwa uhalifu wa kivita walioufanya Afghanistan.

Urusi imetangaza rasmi inaondoa saini yake katika mkataba wa Roma ikisema mahakama ya ICC imeshindwa kutimiza matumaini ya Jumuiya ya kimataifa, haiko huru na ina mapendeleo. Mwaka 2000, Urusi ilitia saini mkataba huo wa Roma lakini haikuidhinisha rasmi mkataba huo.

Rais wa Urusi Vladimir Putin ametia saini agizo la kujiondoa kutoka kwa mkataba wa Roma baada ya nchi hiyo kutofurahishwa na jinsi ICC inavyochunguza kesi ya vita kati ya Urusi na Georgia vya mwaka 2008. Mkataba wa Roma una nchi wanachama 120.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba