ICC yatoa waranti wa kukamatwa mke wa Gbagbo
23 Novemba 2012Bibi Simone Gbagbo anakuwa mwanamke kwa kwanza kushtakiwa na Mahakama ya ICC, huku muwewe Laurent Gbagbo akiwa tayari The Hague tangu Novemba mwaka uliopita, akisubiri kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili ya uhalifu wa kivita. Waranti huo uliotolewa Februari 29, mwaka huu, umewekwa hadharani jana Alhamisi, ambapo unaonyesha kuwa Simone anahusika na mauaji, ubakaji na aina nyingine za unyanyasaji wa kijinsia na vitendo vingine visivyo vya kibinaadamu pamoja na utesaji, wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi wa urais kati ya mwaka 2010 na 2011, ambapo kiasi watu 3,000 waliuawa.
ICC yataka ushirikiano zaidi
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Fatou Bensouda amewataka viongozi wa Cote d'Ivoire kuendelea kutoa ushirikiano na kumfikisha Simone kwenye mahakama ya ICC. Waranti huo unamtuhumu Bibi Simone ambaye kwa sasa yuko nchini Cote d'Ivoire kwa kushiriki kuandaa na kuchochea ghasia hizo. Kwa mujibu wa waranti huo, Simone alikuwa karibu na mumewe, ingawa hakuchaguliwa, alikuwa akijivunia dhidi ya mumewe na alitumia madaraka ya mumewe na kutoa maamuzi ya nchi.
Ghasia katika taifa hilo la Afrika Magharibi ziliibuka baada ya Gbagbo kukataa kuachia madaraka baada ya kushindwa katika uchaguzi wa urais dhidi ya mpinzani wake Alassane Ouattara, rais wa sasa wa Cote d'Ivoire. Taarifa zinaeleza kuwa Simone tayari amefunguliwa mashtaka nchini kwake, kwa kuhusika na mauaji ya halaiki, uhalifu wa umwagaji damu, kuwa kitisho kwa usalama wa taifa na uhalifu wa kiuchumi.
Cote d'Ivoire yakiri kupokea taarifa hizo
Msemaji wa serikali ya Cote d'Ivoire, Bruno Kone, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wamepokea taarifa hizi na sasa wataiangalia hali jinsi ilivyo na kisha kufanya maamuzi. Kone, amesema kwa sasa Simone yuko katika kizuizi cha nyumbani kwenye mji wa Odienne uliopo kaskazini-magharibi mwa nchi hiyo. Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch limefurahishwa na hatua hiyo ya Mahakama ya ICC, lakini limesema ni lazima uamuzi huo ufatiwe na kukamatwa kwa wafuasi wa Ouattara, kwani inadaiwa na wao walihusika na mauaji.
Hata hivyo, Bensouda amesema kuwa waranti zaidi wa kukamatwa watu utatolewa na kwamba ofisi yake inaendelea na upelelezi wake kuhusu uhalifu wote unaodaiwa kufanywa na pande zote mbili. Amesema maombi ya kukamatwa yatawasilishwa kwa majaji mara baada ya kukusanya ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo.Simone na mumewe Laurent Gbgabo walikamatwa kwenye handaki Aprili mwaka 2011, baada ya wanajeshi wa rais wa sasa wakiungwa mkono na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa kuanzisha msako mkali dhidi yao, baada ya kujificha ndani ya Ikulu ya rais.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman