ICC yatoa waranti mpya dhidi Ntaganda
14 Julai 2012Mahakama pekee ya kudumu duniani inayowahukumu wahalifu wa kivita , iliyo na makao yake makuu mjini The Hague, imetangaza kuwa imetoa waranti dhidi ya Sylvestre Mudacumura, kiongozi wa waasi wa Kihutu kutoka Rwanda anayeishi katika jamhuri ya kidemokrasi ya Congo.
Pia imetoa waranti mpya wa kukamatwa Bosco Ntaganda, jenerali laghai wa Kitutsi raia wa Congo , ambaye amepewa jina la utani , "Mharibifu", ambaye ameanzisha uasi unaoendelea sasa katika eneo la mashariki ya nchi hiyo akilitumia kundi linalofahamika kama M23.
Serikali zashutumiana
Serikali mjini Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kutoa fedha kwa kundi hilo, pamoja na silaha na vikosi vya jeshi kuwasaidia wanamgambo wa Ntanganda, ambao wamekamata miji kadha katika jimbo la Kivu ya kaskazini katika siku za hivi karibuni na sasa linaonekana kuwa linatishia kuukamata mji mkuu wa jimbo hilo Goma.
Ntaganda , ambaye ana umri wa karibu miaka 41, anatuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu, kuanzia Septemba mosi mwaka 2002 hadi mwishoni mwa Septemba 2003, katika muktadha wa mzozo katika eneo la Kivu, imesema mahakama hiyo ya ICC.
Mahakama hiyo tayari ilishatoa waranti dhidi ya mbabe huyo wa kivita mwaka 2006 kwa kuwatumia watoto katika jeshi lake lakini katika mwezi wa Mei iliongeza mashtaka mengine.
Mahakama ya ICC imesema kuwa Ntaganda anadaiwa kubeba jukumu la mashtaka matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na manne ya uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji , ubakaji na utumwa wa ngono , mateso na uporaji na utekaji nyara.
Mzaliwa wa Rwanda
Ntaganda alizaliwa nchini Rwanda na alikuwamo katika jeshi la Rwandan Patriotic Forces, lililokuwa linaongozwa na rais wa sasa Paul Kagame, ambalo lilimaliza mauaji ya kimbari mwaka 1994 yaliyofanywa na Wahutu wenye msimamo mkali dhidi ya Watutsi walio wachache nchini Rwanda.
Wataalamu wanasema kuwa Ntaganda , ambaye alijumuishwa katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na kundi lake la waasi wa Kitutsi katika makubaliano yaliyoshindwa ya mwaka 2009, alijitoa katika jeshi hilo Aprili mwaka huu wakati serikali mjini Kinshasa ilipokiondoa kikosi chake kutoka katika maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini.
Serikali ya Kinshasa na ripoti ya wataalamu wa umoja wa mataifa inasema kuwa kuna ushahidi mkubwa wa ushiriki wa Rwanda katika uasi wa kundi la M23, dai ambalo Rwanda inakana.
Umoja wa mataifa na viongozi wa eneo hilo wamewataka viongozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kukaa chini na kufikia makubaliano ambayo yatazuwia kuongezeka kwa vita hivyo katika eneo la Kivu ya kaskazini ambalo tayari limeathirika kwa vita, ambapo vita vya hivi sasa vemesababisha mamia kwa maelfu ya watu kukimbia makaazi yao.
Mahakama ya ICC ilikataa ombi la kwanza la kutoa waranti dhidi ya kukamatwa kwa Mudacumura mwezi Mei lakini hatimaye mahakama hiyo ilitoa waranti siku ya Ijumaa, wakati mbinyo ukizidi katika pande zote mbili kwa ajili ya kufikia suluhisho la kidiplomasia katika mzozo huo wa Kivu.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Idd Ssesanga