1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC yatishia kuwawajibisha viongozi wa mapigano Libya

Daniel Gakuba
16 Aprili 2019

Mwendeshamashtaka mkuu wa ICC ametishia kuzidisha uchunguzi kwa viongozi wa pnde zinazohasimiana Libya, baada ya taarifa kuwa idadi ya waliokufa imepindukia 140, na wengine 18,000 wameyakimbia makaazi yao.

https://p.dw.com/p/3Gtul
Libyen Zusammenstößen zwischen Haftars Streitkräften und den GNA-Streitkräften
Picha: picture-alliance/AA/H. Turkia

Takwimu hizo za hasara iliyosababishwa na uhasama mpya uliozuka nchini Libya zimetolewa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, akinukuu ripoti ya shirika la kimataifa la kuwashughulikia wahamiaji, IOM.

Ripoti hiyo inasema raia 13 ni miongoni mwa watu 146 waliokwishauawa katika mapigano hayo yaliyoanza Aprili tano, lakini Dujarric ameeleza bayana kuwa idadi hiyo ni ya wale tu ambao vifo vyao vimethibitishwa, ikimaanisha kuwa yawezekana idadi ya wahanga wa vita hivyo ni kubwa zaidi.

Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa amesema wahamiaji wasiopungua 3000 wamenaswa katika vituo walimozuiliwa, ambavyo vipo karibu na uwanja wa mapambano, ametoa rai kwa pande zinazohusika kujizuia.

USA Sprecher des UN-Generalsekretärs Stéphane Dujarric in New York
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane DujarricPicha: Imago/ZUMA Press/M. Brochstein

''Tunazitolea mwito pande zote zinazohusika kusitisha uhasama, ili angalau tuweze kuwafikishia msaada wa kibinadamu watu wanaouhitaji mjini Tripoli. Tunapata taabu kubwa kuwafikia watu, kwa sababu magali ya kubeba wagonjwa na ya wafanyakazi wa afya yameshambuliwa, na hilo halikubaliki. Tunataka pande zote kurudi katika kutafuta suluhisho la kisiasa.'' Amesema msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric.

Mwendeshamashtaka wa ICC yaingilia kati

Akizungumza mji The Hague leo, mwendeshamashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifi -ICC Fatou Bensouda amesema hatosita kupanua uchunguzi wa mahakama hiyo juu ya uwezekano wa kutokea uhalifu ambao uko katika wajibu wa mahakama hiyo kuufanyia kazi.

Haya yanajiri wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likijadili muswada uliowasilishwa na Uingereza, unaohimiza usitishaji wa mapigano mara moja nchini Libya. Muswada huo unazema mashambulizi yaliyofanywa na vikosi vitiifu kwa mbabe wa kivita anayedhibiti eneo la Mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar, ni kitisho kwa uthabiti wa Libya, na yanahujumu mpango wa Umoja wa Mtaifa wa kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Libya.

Libya yaililia Ulaya

Wakati huo huo serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa imeomba msaada wa Umoja wa Ulaya kuzuia mashambulizi ya vikosi vya Khalifa Haftar, ikisema utengamano nchini Libya pia ni kwa maslahi ya Ulaya.

Makamu wa rais wa serikali hiyo yenye makao makuu mjini Tripoli Ahmad Maitig, amesema hata hivyo kuwa matarajio ya vikosi hivyo kuukamata kirahisi mji huo mkuu yameishia kuwa ndoto.

Baraza la  usalama la Umoja  wa Mataifa  linatafakari azimio lililoandikwa  na  Uingereza  ambalo  linadai  kusitishwa mapigano nchini  Libya  na  kuzitaka  nchi zote zenye ushawishi kwa pande  hizo  kuhakikisha  zinayatekeleza.

afpe,ape