ICC yamtia hatiani Katanga kwa kusaidia mauaji
7 Machi 2014Katanga alikuwa anakabiliwa na mashitaka kadhaa yakiwemo yale ya kufanya mashambulizi dhidi ya kijiji cha Bogoro tarehe 24 Februari 2003, ambapo watu 200 waliuawa.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Bruno Cetto alisema bila ya msaada wa silaha alioutoa Katanga, makamanda waliofanya mauaji hayo ya Bogoro wasingeliweza kufanya mauaji hayo. Hata hivyo, mahakama hiyo imemuondolea hatia ya kushiriki moja kwa moja kwenye mauaji hayo.
Hii ni ya tatu kutolewa na ICC tangu kuanza kwake kazi zaidi ya miaka 11 iliyopita, na pia itakuwa ni mara ya kwanza kwa mashitaka yanayohusiana na unyanyasaji wa ngono kuingizwa kwenye kesi.
Katanga, mwenye umri wa miaka 35 alianza kufikishwa mahakamani miaka minne iliyopita, akikabiliwa na mashitaka saba ya uhalifu wa kivita yakiwemo ya mauaji, utumwa wa kingono na ubakaji na jukumu lake binafsi kwenye.
Mauaji ya Bogoro yalivyofanyika
Waendesha mashitaka walisema kwamba kiongozi huyo wa waasi aliyewahi kufahamika kwa jina la "Simba" na wapiganaji wake wa makabila ya Ngiti na Lendu walikivamia kijiji hicho cha Bogoro, ambacho kilikuwa kikikaliwa na watu wa kabila la Hema kaskazini mashariki mwa Kongo, wakiwa na bunduki, makombora ya kurushia maguruneti na mapanga, ambapo waliwaua kiasi cha watu 200.
Upande wa mashitaka ulisema kwamba mashambulizi hayo yalidhamiria kukiangamiza kabisa kijiji hicho cha Bogoro. Katika uvamizi huo, wanajeshi watoto walitumika huku wanawake na wasichana wakitekwa na kutumika kama watumwa wa kingono, wakilazilimishwa kuwapikia na kuheshimu amri za wanajeshi wa FRPI.
Mwaka 2004, Katanga aliteuliwa kuwa jenerali kwenye jeshi la serikali ya Rais Joseph Kabila kama sehemu ya sera za kukomesha mgogoro wa kiraia, nafasi ambayo aliishikilia hadi pale serikali ilipomtia nguvuni mwaka 2005.
Katanga alipelekwa mjini The Hague, Uholanzi, mwezi Oktoba 2007 na kesi yake, pamoja na ya mtuhumiwa mwenzake Mathieu Ngudjolo Chui, ilianza miaka miwili baadaye.
ICC yakosolewa
Lakini kesi zao wawili hao zilitenganishwa Novemba 2012, na mwezi mmoja baadaye majaji wakamfutia kesi Ngudjolo wakisema kwamba upande wa mashitaka ulikuwa umeshindwa kuthibitisha ikiwa mtuhumiwa huyo alikuwa na dhima yoyote ya kutoa amri katika mashambulizi ya kijiji cha Bogoro.
Wakosoaji wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wanasema imekuwa ikiendesha mchakato wake kwa kasi ndogo sana na hivyo kuchelewesha haki kwa washukiwa na wahanga wa uhalifu.
Kwa upande mwengine, mataifa ya Kiafrika inaituhumu kwa kushitaki makosa yanayofanyika kwenye bara hilo tu, huku maafa kama yale yanayotokea Mashariki ya Kati na kwengine duniani yakiachwa bila kufuatiliwa.
Kwa vyovyote vile, hukumu hii dhidi ya Katanga inachipukia kwenye moja ya migogoro inayomwaga damu nyingi sana katika eneo lenye utajiri wa madini barani Afrika.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo