ICC yamhukumu Al Hassan kwa uhalifu wa kivita
26 Juni 2024Al HassanAg Abdoul Aziz mwenye umri wa miaka 46, alipatikana na hatia ya makosa hayo ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na mateso, ubakaji na utumwa wa kingono na kuharibu majengo ya kidini na kihistoria.
Jaji aliyesimamia kesi hiyo Antoine Kesia-Mbe Mindua amesema Al Hassan alihusika katika visa vya kuwakata watu sehemu zao za mwili na kuwapiga watu viboko wakati alipokuwa mkuu wa polisi na wakati pia wanamgambo walio na itikadi kali walipoudhibiti mji wa Timbuktu kwa takriban mwaka mmoja kuanzia mwaka 2012.
Mji wa kihistoria wa Timbuktu wazingirwa na wanamgambo
Hatua ya namna atakavyokitumikia kifungo chake itatangazwa hivi karibuni. Akiwa amevalia nguo ya manjano na kitambaa cheupe cha kichwa, Al Hassan alikaa kwa utulivu kabisa akiwa amefunga mikono yake wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake kulikochukua takriban masaa mawili na nusu.
Jaji Mindua amesema Al Hassan pia amehojiwa kuhusu mateso yaliyotumiwa kuwalazimisha watu kukiri mambo yasiokuwa ya ukweli.
Wakati wa kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa mwaka 2020, waendesha mashtaka wanasema wananchi wa Timbuktu wameishi kwa hofu, wakitolea mfano kisa cha mtu aliyekatwa mkono baada ya kutuhumiwa kwa wizi.