ICC Yakutana na Wanachama Wake The Hague
20 Novemba 2013Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mashirika ya Kiafrika na yale ya kimataifa yaliyoko Afrika, mahakama ya ICC iliyoko The Hague, inakabiliwa na changamoto muhimu kutoka kwa viongozi wa Afrika. Katika mkutano wao wa mwezi Oktoba, Umoja wa Afrika ulitaka kesi dhidi ya viongozi wa Kenya, ziliahirishwe na kwamba viongozi wote walioko madarakani wanapaswa kupewa kinga ya kutoshtakiwa na mahakama za kimataifa. Hata hivyo, ripoti ya wanaharakati hao, inazitaka serikali za Afrika kukataa kinga ya kutoshtakiwa viongozi walioko madarakani.
Georges Kapiamba, rais wa shirika la kupuigania haki nchini Congo, anasema kinga ya kutoshtakiwa viongozi wa serikali katika Mahakama ya ICC ni kinyume na kanunu za msingi kwamba hakuna mtu aliyeko juu ya sheria. Kapiamba anasema haki ya waathirika na familia zao, haipaswi kukataliwa, kwa sababu watu waliowasababishia mateso wana nafasi za juu za kisiasa. Mkutano huo utakaojadili zaidi kuhusu athari zinazotokana na hatua ya kuwafungulia mashtaka viongozi walioko madarakani, utatoa fursa muhimu kwa Afrika na serikali nyingine, kuthibitisha jinsi zinavyounga mkono jukumu la mahakama ya ICC katika kuhakikisha haki inapatikana.
Mkurugenzi Mkuu wa tume ya kimataifa ya wanasheria nchini Kenya, George Kegoro, anasema kuwa anasema ukiukwaji wa haki za binaadamu unaofanywa na serikali na makundi yenye silaha, unabakia kuwa changamoto kubwa inayowakabili watu wa Afrika. Baadhi ya viongozi wa Afrika wameonyesha msimamo wao kuwa ICC inailenga Kenya. Nchini Kenya kwenyewe viongozi walishindwa kushughulikia ghasia za baada ya uchaguzi na ndipo ofisi ya mwendesha mashtaka wa ICC, ilichukua jukumu la kuanzisha uchunguzi. Tofauti na Kenya, mashtaka mengine ya uhalifu yaliwasiloishwa kwa mahakama ya kimataifa na serikali ambako uhalifu huo ulifanyika au na na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kama ilivyokuwa kuhusu Libya na Darfur nchini Sudan.
Mwanasheria wa wa kimataifa anayehusika na uhalifu na haki katika kituo cha Afrika Kusini, Angela Mudukuti, anasema kuwa mahakama ya ICC ina mapungufu yake, lakini haiilengi Afrika. Uchunguzi mkubwa wa ICC umefanyika kwa sababu serikali za Afrika ziliiomba mahakama hiyo kushiriki. Hata hivyo, mashirika hayo ya kimataifa yamesema kuna undumila kuwili katika utoaji wa haki ya kimataifa, ambao unahitaji kushughulikiwa.
Mkutano huo unaofanyika mjini The Hague, utamalizika tarehe 28 ya mwezi huu wa Novemba.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/HRW
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman