ICC yaanza kesi dhidi ya kiongozi wa waasi wa Afrika ya Kati
12 Oktoba 2021Mahamat Said Abdel Kani, anayetuhumiwa kwa kuwa kiongozi wa kundi la Seleka, alikamatwa na kukabidhiwa mahakama hiyo mwezi Januari mwaka huu kwa ombi lililotolewa na ICC mwaka juzi.
Abdel Kani anatuhumiwa kwa uhalifu uliotendekea mjini Bangui mwaka 2013.
Anakabiliwa na mashitaka 14 yanayosiana na kuweka watu vizuizini na kuwaadhibu wafungwa kwenye maeneo mawili tafauti mjini Bangui.
Waendesha mashitaka wanaiomba mahakama hiyo kuamuwa kwamba ushahidi uliopo unatosha kuwezesha kesi rasmi kusikilizwa.
Mji huo mkuu wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, uliingia kwenye machafuko makubwa mwaka 2013 baina ya kundi la Seleka lililokuwa likiungwa mkono na Waislamu na lililomuangusha aliyekuwa rais wa wakati huo, Francois Bozize, na la anti-Balaka, ambalo liliungwa mkono na Wakristo. Viongozi wawili wa kundi wa anti-Balaka, Alfred Yekatom na Partice-Edouard Ngaissona, tayari wamefunguliwa mashitaka na ICC.