1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC kuchunguza uhalifu Jamhuri ya Afrika Kati

8 Februari 2014

Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC iliyoko mjini The Hague imesema imeanzisha uchunguzi wa awali kuhusu visa vya uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako mauaji ya kidini yameendelea kupamba moto.

https://p.dw.com/p/1B5Xz
Wananchi wakijihami katika ghasia za Bangui(03.02.2014)
Wananchi wakijihami katika ghasia za Bangui(03.02.2014)Picha: picture alliance/AP Photo

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo ya ICC Fatou Bensouda amesema kufuatia ripoti nyingi ambazo ofisi yake imepokea kuhusiana na ukatili wa kupinduki na madai ya uhalifu mkubwa wa kivita unaoendelea katika Jamhuri ya Afrika,ofisi yake imeamua kuanzisha uchunguzi kuangalia hali hiyo.

Hatua hiyo ya Bensouda kuanzisha uchunguzi kuhusiana na umwagaji wa damu ambao umekuwa ukifanyika katika taifa hilo lenye watu milioni 4.6 kwa mwaka mmoja sasa ,unaifikisha kesi nyengine ya Afrika katika mahakama hiyo.

Machafuko yamepamba moto katika Jamhuri ya Afrika ya Kati ambako maelfu ya watu wameuawa na maelfu wengine kukimbia makaazi yao licha ya kuweko kwa majeshi ya Ufaransa na ya Umoja wa Afrika nchini humo kurejesha hali ya utulivu.

Ufaransa ina wanajeshi 1,600 na Umoja wa Afrika umepeleka kikosi cha wanajeshi 5,000 lakini mpaka sasa wameshindwa kukomesha umwagaji damu unaofanyika chini ya misingi ya kidini na kuwapotezea makaazi theluthi moja ya watu wa nchi hiyo

Mwanajeshi wa Ufaransa katika doria Bangui. (30.01.2014 ).
Mwanajeshi wa Ufaransa katika doria Bangui. (30.01.2014 ).Picha: Issouf Sanogo/AFP/Getty Images

Muhanga wa karibuni wa machafuko hayo alikuwa ameanguka hapo jana kutoka kwenye lori lililokuwa katika msafara wa maelfu ya Waislamu waliokuwa wakiukimbia mji mkuu Bangui kwa kuhofia kushambuliwa.

Wakaazi walimkatakata kwa mapanga hadi kufa na kuuacha mwili wake kando ya barabara. Siku ya Jumatano wanajeshi wa serikali walimpiga hadi kufa mshukiwa wa kundi la waasi la Kiislamu la Seleka katika kisa cha kutisha kilichotokea muda mfupi baada ya sherehe za jeshi zilizohudhuriwa na Rais mpya wa muda wa taifa hilo.

Maelfu wakimbia

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa limesema watu 9,000 wengi wao Waislamu wamekimbilia nchi jirani ya Cameroon katika kipindi cha siku kumi zilizopita.

Watoto ni miongoni mwa wakimbizi wa ghasia Bangui.
Watoto ni miongoni mwa wakimbizi wa ghasia Bangui.Picha: Reuters

Mapigano yalizuka katika taifa hilo masikini mwishoni mwa mwaka 2012 baada ya waasi kumng'oa madarakani Rais Francois Bozize ambaye alikuwa madarakani kwa muongo mmoja.

Waasi wa Seleka ambao wengi wao ni Waislamu walimuondoa madarakani mwezi Machi mwaka jana lakini baadhi yao walianza kupora,kuua na kubaka na kiongozi wao Michel Djotodia rais wa kwanza Muislamu nchini humo alishindwa kuwadhibiti.

Umwagaji damu huo umepelekea kuzuka kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi ambapo wanavijiji waliunda makundi ya kujitolea ya Kikristo yanayojulikana kwa jina la "dhidi ya balaka".

Shirika la Madaktari Wasio na Mipaka limesema katika taarifa hapo Ijumaa kwamba umwagaji damu huo katika siku za hivi karibuni umefikia kiwango "kisichovumilika na kisio na kifani"Mratibu wa misaada ya dharura wa shirika hilo Martine Flokstra amesema "raia wanaendelea kuwa katika hofu ya maisha yao na kwa kiasi kikubwa wametelekezwa wajishughulikie wenyewe."

Tukio la Jumatano la wanajeshi kumpiga hadi kufa anayetuhumiwa kuwa muasi muda mfupi baada ya rais mpya wa mpito Catherine Panza kuzungumzia fahari yake kuona jeshi la ulinzi likitowa mchango wake tena katika usalama wa taifa limezusha fadhaa kubwa katika jumuiya ya kimataifa.

Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza.
Rais wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Catherine Samba-Panza.Picha: Reuters

Mbele ya waandishi wa habari kadhaa ambao walikuwa wakirepoti juu ya sherehe hizo za jeshi,wanajeshi waliovalia sare za kijeshi walimzunguka mtu huyo anayetuhumiwa kuwa muasi wa Seleka na kuanza kumtembezea kipigo.

Mwanajeshi mmoja alionekana akiisukumizia maiti hiyo jiwe kubwa la zege wakati ilipokuwa ikiburuzwa barabarani.Baadae umma wa watu waliichoma moto maiti hiyo na wengine wakipiga picha nayo.

Wafikishwe mbele ya sheria

Waziri Mkuu wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Andre Nzapayeke amesema katika mkutano na waandishi wa habari hapo Ijumaa "Waheshimiwa mawaziri,wasakeni na muwafikishe mbele ya sheria." Akikusudia waasi ambao amesema wametanda kwenye mitandao na kutamba kwenye kamera jambo linalofanya watambulikane.

Waziri Mkuu wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Andre Nzapayeke.
Waziri Mkuu wa mpito wa Jamhuri ya Afrika ya Kati Andre Nzapayeke.Picha: Getty Images

Maelfu ya watu wameuwawa katika nchi hiyo ambayo ni kubwa kuliko mkoloni wake wa zamani Ufaransa juu ya kwamba takwimu halisi hazijulikani katika mzozo ambao kwa kiasi kikubwa kile kinachotokea nje ya mji wa Bangui hakijulikani.

Bensouda amesema hali ya wananchi wa Jamhuri ya Afrika ya Kati imetoka kuwa mbaya na kuwa mbaya zaidi.Ameongeza kusema madai yanayotolewa ni pamoja na mauaji ya mamia ya watu,vitendo vya ubakaji na utumwa wa ngono, uharibifu na uteketezaji wa mali, utesaji,kulazimisha watu kukimbia makaazi yao na kutumia askari watoto.

Amesema "Katika visa vingi , inaonekana wahanga hulengwa kwa makusudi kwa misingi ya kidini."

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC Fatou Bensouda.
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC Fatou Bensouda.Picha: AFP/Getty Images

Repoti za wafanyakazi wa mashirika ya misaada kutoka katika miji kadhaa ilioko ndani nchini humo wamezungumzia juu ya mashambulizi yanayofanywa na makundi ya wapiganaji yakiuwa na kupora bila ya kuwepo mtu wa kuwazuwiya.

Hii si mara ya kwanza kwa mahakama ya ICC kufanya uchunguzi Jamhuri ya Afrika ya Kati ambapo mwaka 2007 mwendesha mashtaka mkuu wa zamani wa mahakama hiyo Luis -Moreno Ocampo alianzisha uchunguzi wa umwagaji damu uliopelekea kukwamatwa kwa makamo wa kwanza wa rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo Jean- Piere Bemba.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP

Mhariri. Caro Robi