1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ICC kuamua kuhusu hatma ya kesi ya Ruto na Sang

5 Aprili 2016

Makamu wa rais wa Kenya William Ruto na mwandishi habari Joshua Arap Sang wanaandamwa na mashtaka matatu ya uhalifu kuhusu vurugu za baada uchaguzi wa Kenya 2007

https://p.dw.com/p/1IPWD
William Ruto Makamu wa rais wa Kenya akiwa ICC The Hague septemba 2013
William Ruto Makamu wa rais wa Kenya akiwa ICC The Hague septemba 2013Picha: Michael Kooren/AFP/Getty Images

Majaji wa mahakama ya ICC mjini The Hague nchini Uholanzi wanatarajiwa kutoa uamuzi wa maandishi(05.04.2016) kuhusiana na ikiwa hoja za watuhumiwa wawili makamu wa rais wa Kenya William Ruto pamoja na mwandishi habari Joshua Arap Sang za kutaka kesi dhidi yao itupiliwe mbali zina msingi au la na hivyo uamuzi wa majaji hao utatoa muelekeo ikiwa wawili hao wanabidi kujibu mashataka au kufutiwa mashtaka yanayowakabili ambayo ni ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Ruto mwenye umri wa miaka 49 na Sang mwenye umri wa miaka 40 wamekanusha mashtaka matatu dhidi ya uhalifu wa kibinadaamu ambayo ni pamoja na mauaji,kuwahamisha kwa nguvu na kuwatesa watu baada ya uchaguzi ulioibua mvutano mkubwa mwishoni mwa mwezi wa Desemba mwaka 2007 na kupelekea vurugu zilizosambaa nchi nzima mapema mwaka 2008.

Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou Bensouda
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC Fatou BensoudaPicha: Reuters

Waendesha mashataka wa mahakama ya Icc wanasema zaidi ya watu 1300 waliuwawa na kiasi ya wengine 600,000 waliachwa bila makaazi katika ghasia hizo mbaya kabisa kuwahi kutokea nchini Kenya tangu nchi hiyo ilipojipatia uhuru wake mwaka 1963 kutoka Uingereza.

Ikumbukwe kwamba kesi hii ambayo inafuatiliwa si tu nchini Kenya lakini hata nje ya mipaka ya taifa hilo la Afrika Mashariki ni kesi ambayo imesababisha kampeini ya viongozi wa ngazi za juu ya kuipinga mahakama ya Icc miongoni mwa mataifa ya Kiafrika huku wengi wa viongozi wa bara hilo wakiishutumu kuwa ni chombo kinachoendesha shughuli zake kwa misingi ya upendeleo na hasa ikijikita katika kuwaonea waafrika.Nchi kadhaa za Kiafrika zimetishia kujiondoa katika mkataba wa roma uliosababisha kuundwa kwa chombo hicho mnamo mwaka 2002 kilichokuwa na lengo hasa la kuwashughulikia wahalifu wakubwa wa vita duniani.

Msimamo wa Kenya

Serikali ya Kenya kwa muda mrefu imekuwa ikishikilia kwamba mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao yatupiliwe mbali kufuatia mahakama hiyo kuchukua uamuzi kama huo katika kesi iliyokuwa ikimuandama rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta.

Mwandishi wa habari Joshua arap Sang anayeshtakiwa pamoja na makamu wa rais wa Kenya
Mwandishi wa habari Joshua arap Sang anayeshtakiwa pamoja na makamu wa rais wa KenyaPicha: picture-alliance/dpa

Mwaka 2014 katika hatua ambayo ilionekana kuwa kipigo kikubwa kwa mahakama hiyo ya Icc mwendesha mashtaka mkuu Fatou Bensouda aliitupilia mbali kesi dhidi ya Kenyatta.Hata hivyo licha ya upande huo wa mashtaka kutaka kuendelea na kesi dhidi ya Ruto mawakili wa makamu huyo wa rais wa Kenya waliwasilisha muswaada maalum wa kisheria wakitaka kesi hiyo itupiliwe mbali kwa hoja kwamba waendesha mashtaka hao wa icc wameshindwa kuthibitisha dhima ya Ruto katika vurugu hizo za baada ya uchaguzi nchini Kenya.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Gakuba Daniel