ICC hailiandami bara la Afrika
18 Oktoba 2013Rais wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu-ICC, Jaji Sang-Hyun Song, amesema mahakama hiyo haijawahi kuilenga nchi yoyote ile ya Afrika. Kauli hiyo ameitoa katika kujibu tuhuma zilizotolewa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwamba ICC ina upendeleo na ubaguzi.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Rais wa Mahakama ya ICC iliyopo The Hague, Uholanzi, Jaji Sang-Hyun Song, amesema mahakama hiyo haijawahi kuifatilia nchi yoyote ile ya Afrika na kuyaita madai hayo kuwa ni ya kusikitisha.
Katika mkutano wake mwishoni mwa juma lililopita nchini Ethiopia, Umoja wa Afrika uliitaka Mahakama ya ICC kufuta kesi ya uhalifu dhidi ya ubinaadamu inayowakabili Rais Kenyatta na Makamu wake, William Ruto.
ICC haipaswi kulaumiwa
Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa Bucharest kuhusu ICC ulioandaliwa na serikali ya Romania, Song ameitetea mahakama hiyo, akisema haipaswi kulaumiwa kwa kile ambacho haijakifanya. Amesema kati ya mizozo minane iliyotokea, kesi tano zilipelekwa ICC na serikali za nchi na kesi mbili zilipelekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kenya ni nchi pekee ambapo ICC ilianzisha uchunguzi wake mwenyewe.
Rais huyo wa ICC amesema bunge la Kenya lilipiga kura mara mbili kupinga wazo lililopendekezwa na jumuiya ya kimataifa la kuunda mahakama maalum ya uhalifu, ambayo itasikiliza kesi kama hizo, lakini kutokana na kushindikana huko, hakukuwa na njia nyingine zaidi ya waendesha mashtaka wa ICC kuingilia kati.
Kenyatta na Ruto wameshtakiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu kwa madai ya kupanga ghasia za kikabila zilizosababisha watu 1,100 kuuwawa na wengine zaidi ya laki sita kukosa makaazi, baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Baada ya kuungana kisiasa na kushinda katika uchaguzi wa mwaka huu, viongozi hao wawili wanadai kuwa kesi dhidi yao inakiuka uhuru wa Kenya na inawazuia kutimiza shughuli zao za kuiongoza nchi hiyo. Hata hivyo, Song anasema wakati waendesha mashtaka wa ICC walipoanzisha uchunguzi, walipewa baraka zote na serikali ya Kenya, wananchi wake na jumuia ya kimataifa.
Ruto ataka kesi yake iahirishwe
Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto ametaka kesi dhidi yake iahirishwe kwa muda wa mwaka mmoja, hadi hapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakapopitisha uamuzi wake. Ruto amesema ataendelea kushirikiana na Mahakama ya ICC, licha ya kutolewa wito wa kuahirishwa kwa kesi yake, ambapo pia anataka kuahirishwa huko ili aweze kupambana na ugaidi. Amesema wanataka uamuzi wa mahakama iruhusu kesi hiyo iendelee bila ya yeye kuwepo mahakamani.
Mbali na kesi ya Kenya, ICC inachunguza kesi za Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Sudan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Libya, Cote d'Ivoire na Mali.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFPE
Mhariri:Yusuf Saumu