IAEA yapitisha azimio kali dhidi ya Iran:
13 Machi 2004Matangazo
VIENNA: Baada ya mashauriano ya siku kadha, Shirika la Kimataifa la Kinyuklea limewafikiana kupitisha azimio kali dhidi ya Iran. Azimio hilo linalaumu kuwa serikali mjini Teheran haishiriki kama inavyotakiana katika juhudi ya kufafanua programu yake ya kinyuklea. Hata hivyo uamuzi wa kufikishwa azimio hilo mbele ya Baraza la Usalama umeakhirishwa hadi kifanyike kikao kijacho cha Shirika la Kimataifa la Kinyuklea hapo mwezi wa Juni. Azimio hilo lilitanguliwa na uamuzi wa Iran wa kusitisha kila aina ya ukaguzi wa programu yake ya kinyuklea na shirika hilo la kimataifa. Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya hapo awali zilishikilia kuwa Iran ipitishiwe azimio hata kali zaidi. Marekani inaishutumu Iran kuwa na mipango ya kuunda silaha za kinyuklea.