1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

IAEA yaelezea wasiwasi juu ya mipango ya nyuklia ya Iran

27 Februari 2024

Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki IAEA limeelezea wasiwasi wake kuhusu uwezo wa Iran wa kutengeneza silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/4cv44
Mfanyikazi wa Iran akishughulikia kinu cha nyuklia cha Isfahan UCF.
Mfanyikazi wa Iran akishughulikia kinu cha nyuklia cha Isfahan UCF.Picha: AP/picture alliance

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki Rafael Grossi amesema Tehran haijatoa maelezo juu ya uwepo wa chembechembe zaidi za madini ya Urani katika vinu vyake viwili vya nyuklia.

IAEA imeeleza kuwa, Jamhuri hiyo ya Kiislamu imeongeza hifadhi yake ya madini ya Urani wakati inaendelea kuwazuia wakaguzi kufikia maeneo yake ya vinu vya nyuklia.

Shirika hilo la Kimataifa la Nishati ya Atomiki limekadiria katika ripoti yake ya robo mwaka kwamba, kufikia Februari 10, madini ya Urani yaliyorutubishwa nchini Iran yamefikia kiwango cha kilo 5,525, sawa na ongezeko la kilo 1,028 tangu ripoti yao ya mwisho iliyotolewa mwezi Novemba mwaka uliopita.

Kwa muda mrefu, Iran imekanusha kuwa inanuia kutengeneza silaha za nyuklia lakini Rafael Grossi ametahadharisha kuwa, nchi hiyo ina kiwango kikubwa cha madini ya Urani yaliyorutubishwa yenye uwezo wa kutengeneza mabomu kadhaa ya nyuklia.