IAEA ina wasiwasi kuhusu vinu vya nyuklia vya Iran
1 Juni 2021Ripoti hiyo ya shirika la kimataifa la atomiki IAEA iliyotolewa imesema Mkurugenzi wa shirika hilo Rafael Grosso pia ameelezea wasiwasi wake kwamba mazungumzo ya pande mbili kati ya shirika hilo na Iran hayakuzaa matunda yaliyotarajiwa. Shirika hilo la uangalizi wa nyuklia la Umoja wa Mataifa limesema pia Iran imeongeza kiwango chake mara 16 zaidi cha uzalishaji wa madini ya Uranium. Mkataba wa nyuklia uliofikiwa mnamo mwaka 2015 kati ya Iran na Marekani, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza, China na Urusi unairuhusu nchi hiyo kuweka malimbikizo ya Uranium yanayofikia jumla ya kilo 202.8 tu.
Soma zaidi:Duru ya nne ya mazungumzo ya mpango wa nyuklia kuanza Vienna
Mpaka sasa ripoti mbili zilizotolewa na Wakala wa Nishati ya Atomiki (IAEA) ni ripoti za kwanza tangu Iran ilipositisha ukaguzi wa vinu vyake vya nyuklia mnamo mwezi Februari. Na kuanzia hapo shirika la IAEA halijaweza kupata data muhimu ili kufuatilia mpango wa nyuklia wa Iran.
Iran ilianza kupunguza shughuli za ukaguzi katika vinu vyake vya nyuklia kwa nia ya kuweka shinikizo kwa serikali ya Rais wa Marekani Joe Biden ili ipate kuviondoa vikwazo vilivyowekwa tena dhidi ya Iran baada ya aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump kuiondoa nchi yake kwenye makubaliano ya nyuklia mnamo mwaka 2018.
Ijapokuwa wiki iliyopita IAEA ilisema kuwa imeongeza muda wa makubaliano yasiyo ya kudumu na Iran hadi Juni 24 ambapo nchi hiyo imeruhusu ukaguzi wa mara kwa mara kuendelea. Mkurugenzi wa IAEA Rafael Grosso amesema kutokana na Iran kushindwa kufafanua maswali ya Wakala wa Nishati ya Atomiki hali hiyo inaathiri sana uwezo wa shirka hilo kutoa uhakikisho wa hali ya mpango wa nyuklia wa Iran kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya ndani na sio kuunda silaha za nyuklia.
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanaendelea mjini Vienna, Austria kuona iwapo Marekani na Iran zinaweza kufikia makubaliano ambapo Iran inatakiwa kupunguza uzalishaji wake wa madini ya Uranium na Marekani kwa upande wake iondoe vikwazo va kiuchumi ilivyoweka dhidi ya Iran.
Vyanzo: AP/DPA/AFP