IAAF: Kenya kushiriki Olimpiki bila wasiwasi
13 Mei 2016Kenya haitaondolewa kwenye mashindano ya olimpiki mwaka huu, licha ya tangazo la shirika la kimataifa linalopiga vita matumizi ya dawa za kutanua misuli miongoni mwa wanamichezo, WADA. Hayo ni kwa mujibu wa shirikisho la kimataifa la riadha IAAF. Tangazo hilo la shirikisho la riadha duniani ni afueni kidogo kwani haijajulikana ikiwa kamati ya Olimpiki inaweza kuingilia kati na ipige Kenya marufuku kwenye Olimpiki!
Kwenye taarifa kwa shirika la habari la Associated Press, shirikisho la riadha duniani limesema kwa kipindi hiki hadi mwaka uishe, Kenya itakuwa katika darubini sawa na mataifa mengine ambayo yameorodheshwa kukumbwa na matatizo ya dawa za kutanua misuli kwa wanamichezo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa licha ya tangazo la shirika la WADA kuwa Kenya haijatimiza matakwa kamili, wanariadha wake wataweza kushiriki mashindano yoyote kitaifa na kimataifa hadi mwisho wa mwaka 2016, wakiwa chini ya uchunguzi.
Hiyo inamaanisha kuwa Kenya itashiriki mashindano ya Olimpiki mwezi Agosti mwaka huu, ila tu ikiwa kamati kuu inayosimamia Olimpiki iingilie kati, hali ambayo ni nadra. Hata hivyo IAAF haikupuuzilia uwezekano wa kamati hiyo kuizuia Kenya, ikizingatiwa kuwa tayari shirika la WADA limeshawasilisha uamuzi wake kwa kamati hiyo.
Wanaotumia mihadarati wakamatwe
Bingwa wa dunia katika urushaji mkuki nchini Kenya Julius Yego ambaye ni Mkenya wa kwanza kuwahi kushinda dhahabu katika kitengo hicho, amesema wanariadha wachache ambao wanatumia dawa hizo wanapaswa kuwajibishwa kwani wanaiharibia nchi jina na sifa. "Sisi wanariadha imetushtua lakini tutaendelea na mazoezi kwa sababu tunajua tuko safi. Ukiwa safi basi hakuna haja ya wasiwasi. Kwa wale wachache wanaotumia nafikiria ni vyema wafungwe jela. Ikiwa Kenya haitaenda Olimpiki basi hatua za sheria zifuatwe dhidi ya wale wametajwa kukiuka sheria za WADA. Wanapasa kuwa kortini maana wanaibisha nchi yetu. Sitaki kufikiria olimpiki bila Kenya hiyo haitakuwa olimpiki itakuwa bure na ambayo haijakamilika".
Shirikisho la riadha duniani IAAF limesema hatua ya WADA kutupilia mbali mswada wa Kenya wa kukabiliana na matimuzi ya dawa hizo, ni dhihirisho ya shirikisho hilo kutaka uwahjibikaji muafaka kitaifa nchini Kenya.
IAAF limeongeza kuwa wanariadha sifika kutoka Kenya ndio sasa wanafanyiwa ukaguzi zaidi kuliko wanariadha kutoka mataifa mengine, na kwamba huenda Kenya ikakumbwa na vikwazo zaidi mwishoni mwa mwaka ikiwa haitatimiza masharti. Tangazo la WADA siku ya Alhamisi lilitaka Kenya kurekebisha vipengee vilivyokuwa na kasoro ndipo itimize matakwa kamili ya shirika hilo kabla ya kuandaliwa kwa michezo ya Olimpiki. Rais wa shirika la WADA Sir Craig Reedie alisema "ninao uhakika maafisa na wengi nchini Kenya watavunjwa moyo na uamuzi huu lakini si vema kwa shirika kuwa na mwanachama wake mmoja mkuu ambaye hafuati matakwa".
Tangu mwaka olimpiki ya mwaka 2012, wanariadha 40 wa Kenya wamepigwa marufuku kwa kutumia dawa za kutanua misuli.
Mwandishi: John Juma/APE/RTRE
Mhariri: Mohammed Khelef