1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IAAF: Kenya haitafungiwa kushiriki Olimpiki

13 Mei 2016

Shirikisho la Kimataifa la Riadha - IAAF kusema kuwa halijawafungia wanariadha wa nchi hiyo kushiriki katika Michezo ya Olimpiki ya Rio

https://p.dw.com/p/1IncV
Symbolbild Doping
Picha: picture-alliance/dpa/G. Breloer

Licha ya wasiwasi mkubwa uliopo kuhusu mpango wa nchi hiyo wa kupambana na matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu.

IAAF imesema Kenya itabakia kwenye orodha ya uchunguzi ya nchi zilizo na matatizo ya matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu miongoni mwa wanariadha hadi mwishoni mwa mwaka huu. Lakini, licha ya uamuzi wa Shirika la Kimataifa la Kupambana na Matumizi ya Dawa za Kuongeza Misuli Nguvu – WADA kuitangaza Kenya kuwa nchi isiyotimiza viwango vyake wanariadha wa Kenya wanaweza kushiriki mashindanoni hadi mwisho wa mwaka huu.

Kwa kuhofia kuwa wangepigwa marufuku, maafisa wa Kenya wanaendelea na harakati za kuyarekebisha mambo wakati waziri wa michezo Hassan Wario amesema kuwa amefahamishwa na WADA kinachotakiwa kufanywa ili nchi hiyo itangazwe kuwa yenye kuzingatia viwango vya kimataifa. Wario amesema bunge litastahili kuitathmini upya haraka iwezekanavyo sheria hiyo na vipengele ambavyo vinastahili kubadilishwa na kuimarishwa. Craig Reedie ni rais wa WADA"Nna uhakika kuwa mamlaka na kila mmoja Kenya atakasirishwa na hatua hii, lakini baada ya kusema hilo, siyo sera nzuri kwa shirika la kimataifa kuwa na mojawapo ya nchi zake kuu isiyozingatia viwango vyetu. Tunatumai kuwa watatimiza viwango haraka iwezekanavyo ili washiriki katika Michezo ya Olimpiki wakiwa na roho safi.

Tangazo hilo limezusha tumbo joto miongoni mwa wanariadha wa Kenya wanaojiandaa kwa ajili ya mashindano ya Olimpiki ya Agosti mjini Rio. Baadhi ya wanaokabiliwa na hatari ya kufungiwa nje ni mwanariadha anayeshikilia rekodi ya dunia katika mbio za mita 800 David Rudisha na washindi wa mbio za mwezi uliopita za London marathon Eliud Kipchoge na Jemima Sumgong.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef