1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hussein Mwinyi ni miongoni mwa wanaotaka urais Zanzibar

17 Juni 2020

Harakati za kuchukuwa fomu za kugombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM zinaendelea baada ya watu wengine watatu kujitokeza akiwemo mtoto wa Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

https://p.dw.com/p/3dw1F
Hussein Mwinyi
Picha: gemeinfrei

Harakati za kuchukuwa fomu za kugombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi, CCM zimeendelea tena leo baada ya watu wengine watatu kujitokeza akiwemo mtoto wa Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa muda mrefu Dokta Hussein Mwinyi ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ulinzi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuwa akitajwa kuwa ni miongoni mwa wagombea wenye nafasi kubwa ya kumrithi Dokta Ali Mohamed Shein anayemaliza muda wake wa urais kikatiba. Mwandishi wetu

Kwa mujibu wa ratiba za wagombea waliokuwa wanachukua fomu leo hii ni Mbwana Yahya Mwinyi na Omar Sheha Mussa. Jina la Hussein Mwinyi halikuwemo katika ratiba iliyotolewa na Chama Cha Mapinduzi, CCM, lakini ghafla taarifa za chini kwa chini zikaanza kusikika kwamba naye ni miongoni mwa watakaojitokeza.

CCM hutangaza jina moja na kumpitisha mgombea ambaye hakutarajiwa na wengi

Muda mfupi baada ya wenzake kukamilisha zoezi la kuchukua fomu, naye akawasili kwenye ofisi za CCM zilizopo Kisiwandui, kuchukua fomu.

Tansania CCM-Anhänger
Wafuasi wa Chama Cha MapinduziPicha: DW/E. Boniface

Mara nyingi CCM huwa wanalitangaza jina moja na kumpitisha mgombea ambaye wengi hawakumtarajia, lakini Dokta Mwinyi ni miongoni mwa wagombea wanaopewa nafasi kutokana na ukaribu wa baba yake na viongozi wa juu akiwemo Rais John Magufuli ambao kwa pamoja ndio wanaojadili majina katika vikao vya maamuzi ndani ya chama hicho tawala.

Wengine waliochukua fomu ni Mbwana Yahya Mwinyi kutoka kwenye Umoja wa Vijana wa CCM, ambaye amesema uamuzi wa kuchukua fomu hiyo sio wa mchezo ni wa dhati kabisa.

Kwa upande wake Omar Sheha Mussa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha katika kipindi cha utawala wa Dokta Salmin Amour pamoja na uzoefu mkubwa aliokuwa nao, anaona bado Zanzibar inamuhitaji mtu kama yeye mwenye uzoefu wa kiuchumi.

CCM inatarajia kuwapitisha wagombea wake wa urais wa visiwani Zanzibar pamoja na Tanzania Bara mapema mwezi ujao. Hata hivyo, wakati wagombea wanaendelea kujitokeza kupitia Chama Cha Mapinduzi kuchukua fomu, kwa upande wa upinzani bado hakuna mgombea ambaye amejitokeza kuchukua fomu ya kugombea urais kwa upande wa Zanzibar.