1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hungary, Poland zapinga mabadiliko ya sheria za Uhamiaji EU

Angela Mdungu
30 Juni 2023

Poland imeiunga mkono Hungary katika kupinga makubaliano ya mabadiliko ya sheria za uhamiaji za Umoja wa Ulaya, hali ambayo imesababisha mvutano katika mkutano wa viongozi wa Umoja huo unaofanyika mjini Brussels.

https://p.dw.com/p/4TGeW
Belgien I EU Summit
Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Nchi hizo zinapinga mabadiliko hayo ya sheria za kuomba hifadhi katika umoja wa Ulaya ambayo upitiaji wake kwa ajili ya marekebisho ulikwama kwa muda mrefu mapema mwezi Juni. Makubaliano hayo yanalenga kugawana waomba hifadhi katika miji mbalimbali ya mataifa ya Umoja wa Ulaya. Nchi zitakazokataa kufanya hivyo zitapaswa kuzilipa zile zitakazowachukua wahamiaji.

Katika mpango huo, Poland na Hungary zilizidiwa kwa kura. Hata hivyo wakati wa mkutano ulioanza Alhamisi, viongozi wa mataifa hayo mawili walikataa kuunga mkono kauli yoyote ya mwisho kuhusu uhamiaji.

Soma zaidi:Nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zimekubalina juu ya mpango wa kuweka sheria kali za uhamiaji.

Kwa mujibu shirika la habari la AFP, Poland iliwataka viongozi waweke kipengele kinachosema kuwa katika masuala nyeti kama vile uhamiaji yanapaswa kuamuliwa kwa kauli ya pamoja, ombi ambalo halikukubaliwa na viongozi wengine wa Umoja wa Ulaya. Baada ya kushindwa kupata muafaka katika siku ya kwanza ya mkutano wao suala hilo linajadiliwa tena leo hii.

Katika hatua nyingine, Viongozi wa Umoja wa Ulaya leo watajadili namna ya kupunguza utegemezi wa mataifa ya umoja huo kwa China.

Mabadiliko ya tabia nchi kujadiliwa 

Wanajadili pia namna ya kuweka usawa kati ya kupunguza hatari na  na kujikita katika masuala mbalimbali kama vile mabadiliko ya tabia nchi.

Lettland I Ministerpräsident I Krisjanis Karins
Waziri mkuu wa Latvia Krisjanis KarinsPicha: Ludovic Marin/AFP

Akizungumzia masuala hayo, Waziri mkuu wa Latvia, Krisjanis Karins amesema wanahitaji kuwa na uwezo wa kupunguza utegemezi wa mataifa ya Ulaya kwa China kwa sababu ya uhusiano unaoendelea kukua kati ya China na Urusi ambao ni tatizo Umoja kwa Ulaya. Hitimisho katika rasimu ya mkutano huo linatoa wito kwa kuishinikiza Urusi kukomesha vita nchini Ukraine na linaonesha wasiwasi kwa mvutao unaoendelea kwenye mlango bahari wa Taiwan.

Soma zaidi:Viongozi wa G7 kujadili "mabavu ya kiuchumi" ya China

Viongozi wa Umoja wa Ulaya watatafuta ya kuonesha umoja wao ingawa tofauti za wazi bado zinaonekana kwa mataifa kama vile Ufaransa na Ujerumani ambayo yana maslahi mapana ya kibiashara nchini China.

Umoja wa Ulaya, wenye nchi wanachama 27, umekuwa ukiichukulia China kuwa mshirika, mshindani na hasimu. Mnamo wezi machi, Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Ursula von der Leyen alisema ili kuibana China, Umoja wa Ulaya unapaswa kupunguza utegemezi wa kiuchumi na kidiplomasia kwa taifa hilo.