'Huna kazi'- Orodha ya waliotimuliwa na Trump
Rais wa Marekani Donald Trump anawaondoa wafanyakazi wa ngazi ya juu wa Ikulu haraka kuliko unavyoweza kutarajia. Ifuatayo ni orodha ya wale waliofutwa kazi na kujiuzulu hadi sasa.
Mtumishi wa karibuni kabisa kuondoka utawala wa Trump: Brett McGurk
Aliteuliwa na mtangulizi wa Trump, Barack Obama mwaka 2015, McGurk alikuwa mjumbe wa Marekani katika muungano wa kupambana na kundi linalojiita Dola la Kiislam. Ilikuwa amalize muhula wake Februari 2019 lakini aliachia ngazi siku chache tu baada ya waziri wa ulinzi Jim Mattis kujiuzulu, kutokana na uamuzi wa ghafla wa Trump wa kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Syria.
Jim Mattis
Waziri wa Ulinzi Jim Mattis alitangaza kustaafu mwishoni mwa Disemba baada ya Trump kupuuza ushauri wake na kuamua kuondoa vikosi vyote vya Marekani nchini Syria. Barua ya kujiuzulu kwa Mattis iliainisha tofauti zilizokuwepo baina yao na ilikosoa jinsi Trump alivyokuwa akiwatendea washirika wa Marekani. Mattis alikuwa muungaji mkono mkubwa wa NATO na washirika wa jadi wa Marekani, tofauti na Trump
Ryan Zinke
Waziri wa mambo ya ndani Ryan Zinke alijiuzulu mwezi Disemba baada ya shinikizo kuongezeka kutokana na uchunguzi uliokuwa ukiendelea kuhusu wadhifa wake na biashara zake. Afisa huyo wa zamani wa jeshi la majini alikuwa mpiga debe mkubwa wa kutanua uwezo wa Marekani wa uzalishaji wa ndani wa nishati kwa kutoa maeneo makubwa ya kuendeleaza utafiti na utafutaji vyanzo vya nishati.
John F. Kelly
Mwezi Disemba, Trump alitangaza kuwa John Kelly, mkuu wa utumishi wa tatu katika Ikulu ya White House ataondoka mwisho mwa mwaka 2018. Alipelekwa Ikulu kwa lengo la kurejesha nidhamu na utulivu lakini inasemekana alihisi kazi hiyo kuwa ya kuchosha na uhusiano na Trump ukawa mchungu. Mick Mulvaney, atachukua wadhifa huo baada ya wengine kadhaa kukataa ombi la kuchukua nafasi hiyo.
Jeff Sessions
Mwanasheria mkuu Jeff Sessions alifutwa kazi mwezi Novemba baada ya miezi kadhaa ya kudhalilishwa na Trump. Licha ya kuwa mpiga debe wa mwanzo mwanzo wa Trump, alijitia kitanzi kwa bosi wake baada ya kujiondoa kutoka kwenye uchunguzi juu ya shaka shaka za ushindi wa rais Trump. Sessions alikuwa mtu wa mstari wa mbele katika kuzitia hila na kuzirudisha nyuma sera za utawala wa Obama.
Nikki Haley
Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Nikki Haley, mmoja ya viongozi wa juu wa wanawake kwenye utawala wa Trump alitangaza kujiuzulu mwezi Oktoba. Alisema kujiuzulu kwake kulipangwa muda mrefu, lakini tangazo lake lilikuwa la ghafla kwa wanasiasa wengi waandamizi. Aliupa utawala wa Trump heshima ya kimataifa kwa kujaribu kwake kutoa kila mara ujumbe sahihi na ulionyooka.
Marc Short
Mkurugenzi wa masuala ya bunge katika Ikulu ya Marekani alitangaza kuwa ataachia wadhifa wake mnamo Julai 20, 2018. Short, mmoja ya wafanyakazi wachache waliodumu kwenye utawala wa Trump, alikuwa pia miongoni wa wale walionekana zaidi akitetea ajenda ya Trump kwenye televisheni. lakini kazi zake zilikuwa zikisitishwa kila mara na rais aliyelalamika kuwa alikuwa akifikia makubaliano dhaifu.
Scott Pruitt
Ilikuwa jambo la kushangaza kwa wengi kuwa ni vipi Pruitt aliweza kudumu kwa muda mrefu kwenye utawala wa Trump, lakini inaonekana rais alimpenda. Wengi kutoka mrengo wa kushoto waliinamisha vichwa kwa kila hatua aliyopiga akiwa mkuu wa wakala wa ulinzi mazingira (EPA). Hata hivyo, Trump alitumia ukurasa wake wa Twitter kumshukuru Pruitt kwa kazi kubwa aliyoifanya alipokuwa akiiongoza EPA.
Ty Cobb
Bobb, mmoja wa mawakili wa ngazi ya juu wa Trump katika uchunguzi unaoendelea kuhusu uingiliaji wa Urusi kwenye uchaguzi wa rais wa mwaka 2016 alisema alihitaji tu kuachana na kazi hiyo kwa kujiuzulu. Lakini wengi wanaamini alilazimishwa na Trump na wengine katika timu yake ya wanasheria kuondoka kwa sababu ya kushindwa kudhibiti kikamilifu uchunguzi wa Robert Mueller kuhusu Urusi.
Tom Bossert
Mshauri wa usalama wa ndani katika Ikulu ya Marekani aliyefanya kazi pia na rais George W. Bush, Tom Bossert, inaripotiwa alifutwa kazi katika panga pangua iliyotokea baada ya John Bolton kuchukua nafasi ya H.R. McMaster kama mshauri wa usalama wa taifa. Inasemekana Bolton hakuwa na tatizo lolote na Bossert, ni kwamba tu alihitaji kikosi kazi chake alipoanza kazi.
David Shulkin
Japokuwa Ikulu ya Marekani ilisema Shulkin alijiuzulu, yeye anasema alifukuzwa. Akitokea utawala wa Obama, aliteuliwa na rais Trump kuongoza wizara ya kushughulikia wanajeshi wastaafu. Mwisho wake ulitokana na kashfa ya gharama za usafiri iliyomuhusisha mkewe. Alikosoa mazingira ya kazi katika utawala wa Trump kuwa "yaliyojaa sumu, yenye vurugu na yasiyo na heshima."
H.R. McMaster
Kwenye ukurasa wa Twitter mwezi Machi 22, 2018, rais Trump alitangaza kuwa anamfuta kazi H.R. McMaster na kumwajiri John Bolton kama mshauri wa usalama wa taifa. McMaster Jenerali anayeheshimika alisema angestaafu kutoka jeshini na kwenye utumishi wa umma. Kuondoka kwa McMaster halikuwa jambo la kushangaza kutokana na kutofautiana na Trump kwenye sera kadhaa.
Rex Tillerson
Mkuu wa zamani wa kampuni ya Exxon, Tillerson alifanya kazi kama waziri wa mambo ya kigeni kwa kiasi mwaka mmoja. Donald Trump alimwondoa Tillerson ili kuunda "kikosi kipya" kuelekea mazungumzo na Korea Kaskazini, akiongeza kuwa Tillerson "hakukubaliana na baadhi ya mambo." Mahusiano baina ya wawili hao yalididimia baada ya kuripotiwa kuwa Tillerson alimwita Trump kuwa "Taahira" mnamo Oktoba 2017.
Gary Cohn
Gary Cohn alifanya kazi kama mshauri mkuu wa masuala ya uchumi wa rais Trump juu ya baraza la uchumi la taifa. Alisaidia pakubwa kupitisha mageuzi tata ya kodi mwaka 2017. Hata hivyo Cohn aliachia ngazi Machi, 2018 baada ya kushindwa kumshawishi Trump kuachana na mpango wa kuzitoza ushuru bidhaa za chuma na bati kutoka nje.
Hope Hicks
Hope Hicks alijiuzulu nafasi yake ya mkurugenzi wa mawasiliano katika Ikulu ya White House mnamo Februari 2018. Siku moja kabla ya kujiuzulu, alitoa ushahidi mbele ya wabunge wa Marekani juu ya uingiliaji wa Urusi kwenye uchaguzi uliopita. Ikulu ya Marekani ilisisitiza kuwa kujiuzulu kwake hakukuwa na uhusiano na ushahidi alioutoa. Hicks alikuwa miongoni mwa wasaidizi wa karibu wa rais Trump.
Rob Porter
Msimamizi wa watumishi katika Ikulu ya White House aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu baada ya wake zake wa zamani kumtuhumu kwa unyanyasaji. Licha ya kujiuzulu, Rob Porter alizitaja tuhuma dhidi yake kuwa uongo mtupu. Hapo kabla Trump alimkingia kifua Porter, na vyombo vya habari vilihoji vipi alipita kwenye uchunguzi wa mwenendo wake kabla ya kuajiriwa.
Stephen Bannon
Bwana huyu alifanya kazi kubwa ya kumfanya Trump ashinde urais wa Marekani, lakini licha ya kuwa mkuu wa mikakati katika kampeni ya Trump na baadae Ikulu Stephen Bannon aliondolewa ndani ya mwaka mmoja. Bannon alikuwa mwasisi wa kaulimbiu ya "Marekani Kwanza." baada ya kushindwa kwa vurugu za watu wanaoshabikia zaidi uzungu huko Charlottesville Agosti, 2018, Bannon alikubali kuondoka mamlakani.
Anthony Scaramucci
Bwana huyu aliyejulikana kwa jina la utani la "Mooch" alikuwa mkurugenzi wa mawasiliano katika Ikulu ya Marekani kwa siku kumi 10 tu. Mwenyeji huyo wa New York aliyejawa bashasha kila wakati alichukua nafasi hiyo ya ndoto yake ambayo kwa miezi kadhaa ilikuwa tupu, lakini alitimuliwa siku ambayo jenerali John Kelly alianza kazi kama mkuu wa utumishi wa Ikulu.
Walter M. Shaub Jr.
Walter Shaub, mkurugenzi wa zamani wa ofisi ya maadili serikalini, alijiuzulu mnamo Julai 2017 baada ya kukabiliana na Ikulu ya Marekani juu ya taarifa za kutatiza za kifedha zinazomuhusu rais Trump. Inaripotiwa Shaub aliuita utawala wa rais Trump kuwa "Kichekesho"
Reince Priebus
Reince Priebus, mkuu wa utumishi wa zamani wa Ikulu ya White House aliamriwa kuondoka miezi sita tu tangu kuchukua wadhifa huo baada ya majibizano ya hadharani na mkurugenzi wa mawasiliano Anthony Scaramucci. Iliripotiwa kuwa Priebus alikuwa miongoi mwa wafanyakazi wa Ikulu ya Marekani waliopinga kuajiriwa kwa Bw. Scaramucci.
Sean Spicer
Sean Spicer, aliyekuwa na mahusiano yasiyopendeza na rais Trump pamoja na vyombo vya habari, alijiuzulu baada ya kumwambia Trump kuwa hakubaliani kabisa na kuteuliwa kwa Bw. Anthony Scaramucci kuwa mkurugenzi wa mawasiliano wa Ikulu ya Marekani.
Michael Dubke
Michael Dubke, mkurugenzi wa mawasiliano katika Ikulu ya Marekani alitakiwa kuachia wadhifa huo mwezi Mei 2017 kutokana na kile kilichodhaniwa kuwa udhaifu wake katika kushughulikia madai ya uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi mkuu wa Marekani.
James Comey
Rais Donald Trump alimfuta kazi mkurugenzi mkuu wa shirika la upepelezi la Marekani FBI James Comey — aliyetuhumiwa kwa jinsi alivyoshughulikia uchunguzi kuhusu kashfa ya baruapepe ya Bi. Hillary Clinton. Hata hivyo wakosoaji wanaamini uchunguzi wa FBI juu ya mafungamano kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi ndiyo ilikuwa sababu halisi.
Michael Flynn
Mshauri wa usalama wa taifa Michael Flynn, alijiuzulu mwezi Februari 2017 baada ya ufichuzi kuwa alijadili vikwazo vya Marekani kwa Urusi na balozi wa Urusi nchini Marekani kabla ya Trump kuingia madarakani, na kisha kumwongopea Makamu wa rais Mike Pence kuhusu mazungumzo hayo.