Hukumu dhidi ya wanaharakati 24 Ethiopia kutolewa leo
13 Julai 2012Kwa mara nyingine tena inaonekana kuwa serikali ya Ethiopia inakwenda kinyume na haki za binadamu. Ethiopia iliyojitangaza kama "Chui wa Afrika", leo hii inawafungwa wengi wanaharakati, waandishi habari pamoja na wapinzani wa kisiasa.
Wakati chuo kikuu cha mjini Addis Ababa wiki iliyopita kilifanya mahafali yake ya kila mwaka , kutokana na sababu za kiusalama hakuna mpiga picha wa binafsi aliyeruhusiwa, baadhi ya Waethiopia wanatikisa vichwa kutokana na jinsi vyombo vya usalama vinavyoichukulia hali ya mambo nchini humo.
Kifungo cha maisha.
Iwapo leo mahakama mjini Addis Ababa itachukua msimamo wa mwendesha mashtaka wa serikali , watahukumiwa waandishi habari pamoja na wanachama wa vyama vya upinzani 24 kifungo cha maisha jela.
Wanashutumiwa kuwa wanaharakati wa chama kinachofanya harakati zake nje ya nchi hiyo cha Ginbot 7, chama ambacho kinaonekana na serikali ya Ethiopia kuwa ni kundi la magaidi. Hali hii inatokana na sheria iliyopitishwa mwaka 2009 ya kupambana na ugaidi, ambapo vyombo vya dola ambavyo vinahusika na ukandamizaji nchini Ethiopia vinapata uwezo wa kuwaandamana watu wanaoikosoa serikali.
Kutokana na kupatikana na hatia mwishoni mwa mwezi Juni, watu hao 24, miongoni mwao akiwemo mwanasiasa wa upinzani Andualem Arage pamoja na mwanablog maarufu Eskinder Nega, serikali ya Ethiopia inaonyesha kwa mara nyingine tena sera zake za kutumia mabavu, kuwa aina yoyote ya ukosoaji utaadhibiwa.
Mwanablog Nega alikamatwa mara baada ya uchaguzi ulioendewa kinyume mwaka 2005, lakini aliendelea kuandika mambo mengi ya kuikosoa serikali katika mtandao wa Internet. Hali hiyo imesababisha sasa kumuingiza matatani.
Laetitia Bader ambaye anafuatilia hali hiyo kwa ajili ya shirika la kutetea haki za binadamu la Human Right Watch akiwa mjini Nairobi amesema.
"Hali ya haki za binadamu iko katika matatizo makubwa , serikali imekuwa ikitumia kila aina ya nyenzo kuzuwia vyombo huru vya habari na haki ya kujieleza na kutoa mawazo. Tuna wasi wasi mkubwa kutokana na ukweli kwamba kati ya watu 34 walioshtakiwa chini ya sheria za kupambana na ugaidi tangu mwaka 2011, kumi na mmoja ni waandishi habari. Kwa hiyo kuna ushahidi kuwa matumizi ya sheria hii ni moja kati ya nyenzo muhimu za kunyamazisha uandishi habari huru na ukosoaji".
Ethiopia kama mtetezi wa Afrika
Ethiopia inajionyesha hivi sasa katika sura mbili tofauti kabisa. Hapa, chui huyu wa Afrika anawavutia wawekezaji kutokana na ukuaji mkubwa wa kiuchumi, ambapo katika mji mkuu Addis Ababa kunachipuka majumba marefu ya ofisi pamoja na mahoteli kila wiki. Hali hii ndio inayompa nafasi waziri mkuu Meles Zenawi kuzungumza kwa niaba ya Afrika katika majukwaa ya kimataifa yanayohusu mazingira, mkutano wa mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi ya G20.
Katika majukwaa haya anazungumzia upinzani wake dhidi ya ukandamizaji kisiasa, mgawanyiko wa kikabila, ughali wa maisha ulipindukia na hali mbaya ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Wafadhili wako kimya
Haya ndio yaliyosababisha mapinduzi katika mataifa ya Afrika kaskazini.Kwa mara ya kwanza wanaharakati walijaribu kufanya upinzani mwaka 2011 chini ya kauli mbiu inayojulikana kama Beka, kwa lugha ya Kiamhara ikiwa na maana" inatosha". Lakini maandamano yao yalikumbana na vyombo vya dola na kuziliwa katika mtandao wa Internet na facebook.
Mbaya zaidi ni kwamba mataifa fadhili kwa Ethiopia ambayo kati ya mwaka 1991 na 2009 waliipatia nchi hiyo kiasi cha dola za Marekani bilioni 24 kwa misaada ya maendeleo, wananong'ona tu katika ukosoaji wao.
Mwandishi : Ludger Schadomsky / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Josephat Charo.