Idadi ya wahanga bado haijulikani
7 Oktoba 2015Shirika hilo lenye makao yake makuu mjini London Uingereza na ambalo linapokea ripoti zake kutoka mitandao na duru kadhaaa za hospitali nchini Syria,linazungumzia mashambulio yaliyofanywa na ndege za Urusi katika maeneo yasiyopungua manne huko Hama na matatu katika mkoa wa Idlib.Mashambulio hayo yaliyotokea alfajiri ya leo "yalikuwa makali kupita kiasi" limesema shirika hilo ambalo halijataja bado kuhusu idadi ya wahanga wa mashambulio hayo.
"Kwa mara ya kwanza hujuma za angani zimefanyika wakati mmoja na mashambulio ya nchi kavu kati ya vikosi vya serikali na waasi" amesema mkurugenzi wa shirika hilo la haki za binaadam la Syria Rami Abdel Rahmane.
Kwa maoni yake mapigano yaliyoripuka Hama,yamesadif wakati vikosi vya serikali yakiwemo makundi ya wanamgambo wanayoiunga mkono serikali ya Bashar al Assad walipoanza kuhujumu vituo vya waasi mnamo wakati ambapo ndege za kivita za Urusi nazo zilikuwa zikiporomosha mabomu toka hewani.
Rami Andel Rahmane ameongeza kusema, "Serikali pia imevurumisha makombora ya nchi kavu katika mkoa huo. "
Haijulikani bado kama vikosi vya serikali vinasonga mbele
Mikoa ya Hama na Idlib imeshawahi kuhujumiwa na ndege za kivita za Urusi,septemba 30 iliyopita pale Urusi ilipoanzisha hujuma za angani dhidi ya makundi ya magaidi wakiwemo wale wa dola la kiislam IS nchini Syria.
"Hatuna bado ripoti kama hujuma hizo zimevisaidia vikosi vya serikali kusonga mbele,lakini tunajua kwamba hujuma za angani zimepiga magari na vituo vya waasi" amethibtiisha mkurugenzi wa Shirika linalosimamia haki za binaadamu nchini Syria Rami Abdel Rahmane.
Uturuki haitaki ugonvi na Urusi
Wakati huo huo Uturuki imependekeza uitishwe mkutano mjini Ankara kati ya maafisa wa kijeshi wa Uturuki na Urusi ili kuepusha balaa la kuvunjwa anga ya Uturuki na Urusi.Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Uturuki Tanju Bilgic amesema balozi wa Urusi mjini Ankara ameitwa kwa mara ya tatu hii leo kwa majadiliano zaidi kuhusu visa viwili vilivyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita pale ndege za kivita za Urusi zilipoingia katika anga ya Uturuki.Bilgic amekanusha ripoti ya vyombo vya habari vya Urusi inayodai kwamba Uturuki imependekeza paundwe tume maalum ya ushirikiano nchini Syria.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman